Home FEDHA Tumia 50/20/30 kuweka akiba

Tumia 50/20/30 kuweka akiba

0 comment 150 views

Kuweka akiba bado ni changamoto kwa watu wengi, licha ya uwepo wa namna mbalimbali za kufanya hivyo. Jambo la msingi ambalo kila mtu anatakiwa kuzingatia ili kufanikiwa katika hili ni kujiwekea malengo. Wengi hushindwa kuweka akiba kutokana na kukosa malengo. Kabla ya kitu chochote, ni vizuri kuwa na malengo (ya muda mfupi na mrefu) ili iwe rahisi kujua unaweka fedha kwa sababu gani.

Zipo njia nyingi za uwekaji wa akiba, lakini hapa nitaelezea kanuni ya 50/20/30. Kanuni hii ni kanuni kongwe, watu wengi wameitumia na kupata mafanikio. Kupitia kanuni hii mtu anatakiwa kupanga matumizi/gharama zake katika vipengele vitatu ambavyo ni kama ifuatavyo:

  • 50% Mahitaji muhimu

Kwa kuanza, unashauriwa kutenga asilimia 50 ya mapato yako ya kila mwezi kwa ajili ya mahitaji yako muhimu ya kila siku kama vile malipo ya umeme, chakula, gesi, mafuta ya gari, marekebisho nk. Kiwango hiki ni kubwa lakini baada ya kuorodhesha mahitaji yako yote, utaona kuwa fedha yote inaisha. Jambo la msingi hapa ni kuepuka mahitaji yasiyo muhimu ili kuepuka kutumia fedha bila mpangilio.

  • 20% Akiba, uwekezaji na malengo

Kuweka akiba ni muhimu na kuwekeza pia ni muhimu ikiwa unataka kufanikiwa katika maisha. Hakikisha unaweka akiba ili kuepuka changamoto mbalimbali. Pia ni muhimu kuwekeza fedha ili ziweze kuongezeka zaidi. Badala ya kuweka fedha benki unaweza kuwekeza fedha hizo katika biashara ndogo au kazi ya ziada ili kutengeneza fedha zaidi. Pia katika kipengele hiki inashauriwa fedha ulizonazo kulipa madeni ili kuepuka historia mbaya ya ukopaji ikiwa utahitaji mkopo baadae.

  • 30% Matumizi mengine

Ni dhahiri kuwa umefanya kazi kwa bidii na kutengeneza kipato chako hivyo si vibaya kutenga asilimia kadhaa za fedha kwa ajili yako. Ni muhimu kwa kila mtu kufurahia mapato yake. Hili linawezekana ikiwa matumizi binafsi yatazingatia ustaarabu na nidhamu ya fedha ili mtiririko wako wa fedha usiathirike na mipango mingine ya muhimu iweze kuendelea kama kawaida.

 Jinsi ya kuanza

Kanuni hii inaweza kupangwa kulingana na mtindo wa maisha, gharama za mahitaji na kipato cha mtu. Sio rahisi kwa sababu siku zote matendo na maneno hutofautiana lakini ikiwa utakuwa makini, kanuni hii itabadilisha mtiririko wako wa fedha kwa kiasi kikubwa. Orodhesha mahitaji yako yote ili kujua fedha zako zinaenda wapu. Hii itarahisisha kujua vitu gani ni muhimu na sio muhimu. Unapofahamu gharama inakuwa rahisi katika upangaji wa bajeti.

Hakikisha kuwa hutumii zaidi ya 50% ya mapato yako kwenye mahitaji muhimu. Inapotokea kuwa imezidi, jaribu kuangalia mahitaji unayoweza kupunguza. Kwa mfano ikiwa umepanga nyumba mbali na sehemu yako ya kazi na unatumia gharama za ziada kwa ajili ya usafiri, basi unaweza kuhama na kukaa maeneo yaliyo karibu na kazini ili kubana matumizi. Kwa upande wa 20%, fedha zinaweza kuwa ndogo kulingana na kipato, lakini jambo hilo lisikukatishe tamaa. Hakikisha unaendelea na kanuni yako na weka fedha zinazosalia katika vipengele vingine hapa.

Kanuni hii inaweza isifanye kazi kwa kila mtu hivyo ni vizuri kujifunza njia nyingine za kuweka akiba. Kutokana na kipato chako, mbinu nyingine zinaweza kufanya kazi vizuri zaidi hivyo endelea kujifunza na kufahamu zaidi ili kuchagua njia sahihi ambayo itakuwezesha kufikia malengo yako.

 

 

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter