138
Mwongozo wa Uwekezaji wa Mkoa wa Geita umezinduliwa jana tarehe 22 Septemba 2019 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa wakati wa Maonyesho ya Teknolojia ya Dhahabu kwenye Uwanja wa Kalangalala Mjini Geita. Zaidi ya watu 1000 walishiriki uzinduzi huo, ikijumuisha viongozi mbalimbali wakiwamo Mawaziri, Wabunge, Wakuu wa Mikoa na Madau wa Madini.
Katika uzinduzi huo Waziri Mkuu alibainisha jitihada mbalimbali ambazo Serikali imefanya kuhakikisha Madini yananufaisha Nchi na Watu wake.
Waziri Mkuu Majaliwa amewaonya watoroshaji Madini na kusema Serikali ipo makini na imejidhatiti vya kutosha na kwamba haitokuwa na huruma nao.
Aidha alisema kwa wale wasiotaka kuelewa na kuacha kutorosha madini Serikali itashughulika nao.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Doto Biteko amesema kwa sasa Serikali na Makampuni yanayomiliki migodi wanaheshimiana kwani Makampuni hayo yanatii magizo na kufuata sheria za nchi.
Waziri Doto amesema kabla ya kufunguliwa kwa masoko ya madini nchini makusanyo ya dhahabu yalikuwa kilo 101 kwa mwezi lakini baada ya masoko kufunguliwa makusanyo yameongezeka na kufikia kilo 1,974 hivi sasa.
Akizungumza mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Dkt. Tausi Mbaga Kida, alisema ESRF chini ya ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na kwa kushirikiana na Serikali imekuwa ikiandaa Miongozo ya Uwekezaji katika Mikoa kwa lengo la kuchambua na kuainisha fursa za uwekezaji zilizopo katika mikoa husika ili kuwavutia wawekezaji.
Dkt. Kida alisema mpaka sasa ESRF imesaidia Mikoa 17 kuandaa Miongozo ya Uwekezaji ambapo mikoa 11 imekamilisha na Mikoa 6 iko katika hatua mbalimbali na kuongeza kuwa ESRF itaendelea kuandaa Miongozo ya Uwekezaji katika mikoa iliyobaki kuanzia mwezi wa kumi mwaka.
Alisema kazi hii ya Uandaaji wa Miongozo ya Uwekezaji imeweza kuibua fursa nyingi kwenye Mikoa husika zikiwa katika sekta na ngazi zote.
“Kwa mfano mheshimiwa Waziri hapa Geita kuna fursa kubwa katika sekta ya madini hasa uchimbaji na uongezaji thamani wa madini ya dhahabu kwa wawekezaji wadogo, wa kati na wakubwa. Fursa nyingine zipo katika sekta ya viwanda, kilimo, ufugaji, uvuvi, ujenzi, utalii, na huduma. Maelezo ya kina juu ya fursa hizo yapo kwenye Mwongozo wa Uwekezaji ambao utauzindua leo hii”alisema Dkt. Kida.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa ESRF Miongozo hii ya Uwekezaji ngazi ya Mikoa itachangia katika Mwongozo wa Uwekezaji wa Taifa na kwamba ESRF itaendelea kushirikiana na mikoa katika utekelezaji wa miongozo hii kwa kusaidia kufanya upembuzi yakinifu (feasibilty studies), kuandaa Miongozo ya Biashara (Business Plans) kwa baadhi ya fursa ambazo mikoa itapenda kuwekeza, na kunadi fursa zilizopo kwenye Miongozo.
Aidha Kida alishukuru wataalamu wa ESRF walioshiriki kuandaa mwongozo huo na kuufanikisha. Aliwataja kwa majina waliofanikisha kuwa ni pamoja na Margareth Nzuki, Dk Oswald Mashindano, Prof. Godwin Mjema; Doris Lyimo na Mussa Mayala Martine.
Mkurugenzi wa ESRF aliwapongeza pia viongozi wa Mkoa wa Geita kwa jitihada zao za kuuweka wazi mkoa huo na kuwataka wadau wote kuhakikisha Mwongozo huo unatumika ipasavyo ili kuleta matokeo yaliyo kusudiwa katika mkoa wa Geita na Taifa kwa ujumla.