Imekuwa ni kawaida kuona kuwa wafanyabiashara hasa wa rejareja wakijumua bidhaa zao kwa wafanyabiashara wa jumla ambao hutoa bidhaa hizo kwa wazalishaji husika ambao huuza bidhaa hizo katika bei nafuu zaidi. Sawa utaratibu huo si mbaya lakini wafanyabiashara wengi wamekuwa wakilalamika kuhusu mchakato huo kutumia muda mrefu hali ambayo inaweza kusababisha wafanyabiashara wapoteze muda na fedha kila inapotokea bidhaa hazijafika katika muda muafaka kutokana na uwingi wa mahitaji ya bidhaa kutoka kwa wafanyaiashara.
Kutokana na hilo, Kampuni ya Azam Group imeweza kupunguza changamoto hiyo hususani kwa wafanyabiashara waliopo Jijini Dar es Salaam kwa kuanzisha Application (programu) iitwayo ‘Sarafu’ ili kuweza kurahisisha mchakato mzima wa ununuzi wa bidhaa za Azam na nyingine zote kupitia simu janja na moja kwa moja kutoka katika kampuni mbalimbali zinazozalisha bidhaa.
Faida ya kutumia programu hii
Licha ya kuwa kupitia programu hii wafanyabiashara wanauziwa bidhaa kwa bei nafuu zaidi kulingana na hali ya soko, kupitia programu hii mteja anauhakika wa kuona bei kamili ya bidhaa anayohitaji kwani kila bidhaa iliyopo kwenye programu hii imeorodhesha na bei yake kamili jambo ambalo si rahisi kukuta kwa wasambazaji wasio rasmi wa bidhaa mbalimbali nchini.
Mchakato mzima wa kuagiza bidhaa katika programu hii hufanyika kidijitali hivyo hakuna haja ya kupiga simu mara nyingi au kusubirishwa huku watu wengine wakihudumiwa. Hii huleta urahisi kwa wafanyabiashara kwani hufanya mchakato huu kwa muda mfupi huku wakiendelea na mambo mengine ili hali wana uhakika wa mzigo mpya wa bidhaa.
Kikawaida si rahisi kwa wasambazaji wa bidhaa wasio rasmi kusema kuwa wameishiwa mzigo na kuwaambia wafanyabiashara wa rejareja wasubirie, lakini mfanyabiashara anayetumia programu hii kuagiza bidhaa anaepukana na changamoto hiyo. Kwani kupitia Sarafu bidhaa zote ambazo bado zipo huonekana moja kwa moja hii husaidia kujua kama bidhaa unayoitaka utaipata katika muda unaohitaji kwani baadhi ya bidhaa huuzika kwa haraka zaidi kuliko nyingine.
Pia suala la fedha ya uwasilishaji wa bidhaa katika eneo husika limetatuliwa kupitia programu hii. Hivyo ‘Deliveries’ za bidhaa hufanyika bure, ili mradi mteja atanunua bidhaa zinazoanzia kiasi cha shilingi 70,000 kwa fedha za Kitanzania. Aidha baada ya kuwasilishiwa bidhaa mteja ana uwezo wa kulipa fedha taslimu au kupitia mtandao.
Mbali na hayo, Kampuni ya Azam Group imepanga kuboresha huduma zinazopatikana katika programu hiyo kadri siku zinavyokwenda kulingana na mahitaji ya wateja wanaotumia programu hiyo. Moja ya huduma ambayo wanafikiria kuiboresha ni suala la mikopo kwa wateja wanaotumia programu hiyo ili kurahisisha ufanisi wa biashara kwasababu si kila siku biashara huenda vizuri.
Progamu hiyo kwa sasa inapatikana katika simu janja yeyote ya Android, ambapo mteja hutakiwa kwenda kupakua programu hiyo kwenye Google store kisha kusajili akaunti yake na kuendelea na matumizi ya programu hiyo kulingana na mahitaji ya biashara yake.