Imekuwa ni kawaida kwa biashara nyingi duniani kupata faida zaidi katika msimu wa sikukuu na likizo ambao huwa ni mwisho wa mwaka, hali hiyo hutokana na wateja wengi kuwa huru kufanya manunuzi ya ziada kwa ajili yao, marafiki, na ndugu. Hivyo katika biashara yeyote kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na mpango maalum ambao utawavutia wateja wengi zaidi kununua biadhaa au huduma husika.
Hizi hapa ni baadhi ya mbinu ambazo zinaweza kusaidia kuongeza mauzo katika msimu huu wa sikukuu na likizo:
Punguzo la bei
Siku zote wateja hufurahia punguzo la bei. Hivyo toa punguzo la bei kwa wateja wako hasa wale waaminifu ili kuweza kuwahamasisha wateja kununua bidhaa au huduma zaidi. Ni dhahili kuwa wateja hupenda kuelezana uzoefu kuhusu bidhaa au huduma mbalimbali. kwa kuwa na punguzo la bei katika msimu wa sikukuu katika biashara yako wateja wengi zaidi watanunua bidhaa zako na kwenda kuwaeleza watu wengine kuhusu punguzo hilo ili waweze kununua bidhaa hizo kwa bei ndogo.
Shirikiana na wafanyabiashara wengine
Ni muhimu kwa wafanyabiashara kushirikiana katika msimu wa sikukuu ili kuweza kupata mafanikio zaidi. Hapa ushirikiano unaweza kufanyika kwa kuwahamasisha wateja wanaoenda katika biashara moja kwenda katika biashara nyingine. Kwamfano mfanyabiashara wa vifaa vya elektroniki anaweza kufanya makubaliano na mfanyabiashara wa chakula na kuwaeleza wateja kuwa wanaweza kupata chakula kizuri kwa bei ndogo baada ya kununua vifaa visivyopungua laki moja, hii inakuwa inasaidia biashara mbili kupata wateja kwa wakati mmoja na ikiwa mteja atafurahia bidhaa au huduma sehemu mbili basi ni rahisi kuwaelekeza watu wengine kwenda katika biashara au kampuni hizo.
Tuma barua pepe kwa wateja
Hii ni nzuri hasa kwa biashara za mtandaoni, ni muhimu kuwajulisha wateja hasa wale ambao ni waaminifu umuhimu wao katika biashara yako. Hivyo angalia historia ya wateja ambao wamekuwa wakifanya manunuzi ndani ya mwaka na kuwatumia barua pepe ya shukrani na kueleza kama kuna maboresho ambayo yatafanyika mwakani, pia si vibaya kuelezea punguzo la bei linalofanyika katika msimu wa sikukuu hii itawakumbusha uwepo wa bidhaa au huduma yako na kuwafanya wahamasike kuja kufanya manunuzi kwako.
Ikiwa kila wakati wanafanya agizo la aina moja ya bidhaa au huduma unayouza unaweza kubinafsisha barua pepe hiyo kwa kutoa maoni kuhusu bidhaa nyingine inayoendana na bidhaa ambazo wamekuwa wakinunua kulingana na historia yao ya ununuzi.
Toa usafirishaji wa bure au maalum
Gharama za usafirishaji wa bidhaa au huduma ni moja ya vitu ambavyo wateja wengi hawafurahishwi navyo katika mchakato mzima wa kununua bidhaa hadi kuipata. Hivyo ili kuweza kuwahamasisha wateja kununua bidhaa katika biashara au kampuni yako unaweza kuweka mpango maalum wa kufikisha bidhaa kwa wateja wako aidha kwa gharama ndogo zaidi au bure kabisa. Pia si vibaya kuwafikishia wateja wako bidhaa zao wewe mwenyewe kama mmiliki ili kuweza kujifunza zaidi kuhusu uzoefu ambao wateja wanaupata kutokana na huduma au bidhaa yako. Hii itasaidia kufanya maboresha mwanzoni mwa mwaka.
Andaa mashindano
Hapa mfanyabiashara anaweza kuandaa mashindano aidha katika eneo biashara au hata katika mitandao ya kijamii kama instagram kwaajili ya wateja ili waweze kushinda zawadi mbalimbali zinazopatikana katika biashara au huduma husika. hii itawahamasisha watu wengi kutembelea biashara yako na hata kununua bidhaa hata kama hawatoshinda. Hakikisha tangazo la shindano hilo lina maelezo sahihi ili wateja waweze kuelewa mambo ya kufanya ili kuweza kushinda.
Aidha, si vibaya kufanya utafiti kuhusu changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii inayokuzunguka na kutoa msaada au suluhisho. Kwasababu mbali na kupata faida mwaka mzima si vibaya kutoa shukrani katika jamii, mchango katika jamii sio lazima uwe ni fedha, usafi wa mazingira, utoaji wa elimu nk ni baadhi ya mambo ambayo yanaweza kufanywa katika msimu wa sikukuu na kuleta picha nzuri kuhusu biashara yako katika jamii inayokuzunguka.