Riba kubwa inayotozwa na taasisi za fedha imetajwa kama moja ya changamoto kwa wananchi wenye kipato cha chini kushindwa kumudu mikopo.
Mbunge wa Vunjo Dk Charles Kimei uwepo wa riba kubwa imekuwa ni faida kubwa ya benki na wanahisani wake lakini kwa wananchi ni maumivu.
Dr Charles Kimei, ambae amewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya CRDB amesema riba ikishuka itasaidia wananchi wengi kukopa kwa wingi na kufanya taasisi za fedha kuwa rafiki na wafanyabiashara.
“Riba ya asilimia 15 ni mateso kwao na ilipaswa jambo hilo lipitiwe na kutazamwa upya ili kuishusha kwa kuwa duniani kote sera ya fedha ni riba sio kingine’ amesema.
Ameeleza kuwa Sera ya fedha Tanzania bado ina upungufu mkubwa kwa kuwa haigusi watu wenye kipato cha chini.
“Sera itakuwa nzuri ikiwagusa watu, lazima tuangalie suala la riba za benki, kwa Sasa ni kubwa mno lazima turudi kwenye single digital (tarakimu moja) ndipo tutafaulu,” amesema Dk Kimei.
Dk Kimei ameeleza hayo Bungeni Dodoma wakati akichangia mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango wa Serikali wa 2022/23 uliowasilishwa na Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba ambapo wanakadiria bajeti ya mwaka ujao iwe zaidi ya Sh39 trilioni.