Home AJIRA Nyongeza ya 8,000 ni dhihaka kwa mfanyakazi: Tucta

Nyongeza ya 8,000 ni dhihaka kwa mfanyakazi: Tucta

0 comment 100 views

Raisi wa Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi TUCTA Tumaini Nyamhokya amesema wamewasilisha malalamiko yao kwa Serikali kwani Kiwango cha nyongeza ya mshahara iliyoongezwa katika mwezi Julai ni kinyume na ahadi iliyotolewa na Rais Samia siku ya Mei Mosi mwaka huu kwani baadhi ya watumishi wamepata nyongeza ya shilingi Elfu Nane na kuendelea.

“Hoja kubwa iliyotuleta ni hiyo, tumeleta kilio cha wafanyakazi kwa serikali ambayo ndiyo imeongeza hiyo mishahara na bahati nzuri wamepokea na wanafanyia kazi, tulitegemea nyongeza itawagusa watumishi wenye vima vyote vya mishahara kwa kiwango kilichozoeleka”

Kwa bahati mbaya kiwango kimekuwa cha chini ambacho kimewaumiza sana wafanyakazi wa nchi hii, kima cha chini cha laki tatu ndo hao wameongezewa 23.3% ambayo inatupeleka kwenye kama Sh 70,000.

Asilimia kubwa ya wenye kima cha juu cha mishahara walichokutana nacho ni Sh 12,000 na wengine wanasema wamekutana na Sh 8,000, kumuongeza mtu Sh 8,000 ambae ana miaka zaidi ya sita saba hajaongezwa mshahara ni jambo ambalo si jema, ni dhihaka kwa mfanyakazi.”

Ameeleza kuwa katika nyongeza hiyo kuna baadhi ya kada hazikuguswa kabisa.

Ameeleza kuwa kuna tofauti kubwa ya nyongeza ambapo wale watumishi wa kima cha chini wamepata nyongeza ya asilimia 23.3 na wale wa kima cha juu ana asilimia 0.6.

“Hii ni tofauti kubwa ambayo haijawahi kutokea, tukumbuke kuwa Rais alilenga kuongeza mishahara, na hakuwa amelenga kuwatoa watu wa daraja Fulani kuwapeleka mahali pengine, kwa iyo kama ni nyongeza ya mshahara inagusa kula ngazi ya mshahara wa mtumishi wa umma,” ameeleza.

Amesema “hata kiwango hichi cha 70,000 ukikitizama pamoja na kwamba tunashukuru angalau kima cha chini kimetizamwa, bado si kiwango halisia kinachomtoa mtumishi kwenye adha za maisha na kulinganisha na maisha aghali yaliyopo sasa.”

Kwa sasa, Serikali imeanza Mazungumzo na Viongozi wa shirikisho la vyama vya Wafanyakazi Nchini Pamoja na Viongozi wa vyama vinavyounda Shirikisho hilo Jijini Dodoma Kwaajili ya kujadili Juu ya sintofahamu iliyojitokeza katika ahadi ya nyongeza ya mshaara ya asilimia 23.3 kwa wafanyakazi iliyoanza kutekelezwa mwezi Julai.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter