Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema ni muhimu kwa taasisi za elimu barani Afrika kulinganishwa na nyingine duniani ili kuongeza weledi na kuzalisha wataalamu watakaoshindani duniani.
Prof. Nombo amesema hayo Septemba 27, 2022 jijini Cape Town, Afrika Kusini wakati akishiriki mjadala wa mada kuhusu ‘Ulinganishaji wa Vyuo Vikuu Afrika: Una maana gani kwa wafadhili wa wanafunzi na Serikali?’ iliyowasilishwa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Cape Town, Prof. Rosina Mamokgethu Phakeng.
“Taasisi za elimu ya juu ni za kidunia na hivyo ni muhimu kuwa na ulinganishaji ili zitambulike duniani, siyo ndani ya nchi zetu au barani Afrika tu,” amesema Prof. Nombo ambaye pia amefundisha na kuongoza taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini.
Mkutano huo wa Tatu wa Kimataifa unajadili kuhusu Ugharamiaji wa Elimu ya Juu barani Afrika uilioandaliwa na Shirikisho la Taasisi za kiserikali zinazotoa Mikopo ya Elimu ya Juu Afrika (AAHEFA) na kuhudhuriwa na washiriki 150 kutoka nchi 11 barani Afrika.