Katika kuendelea na shamra shamra za kusherekea Mwezi wa Huduma kwa Wateja, Benki ya NMB imeipandisha na kuipeperusha bendera yake katika Mlima Kilimanjaro.
Wafanyakazi sita wa Benki hiyo ndio walioipandisha bendera hiyo katika kilele cha Mlima huo mrefu Barani Afrika.
NMB imesema tukio hilo linadhihirisha kuwa wapo tayari kuendelea kutoa huduma bora kwa wateja na umma kwa ujumla, ikiwemo kuwapa masuluhisho mbalimbali ya kifedha na kuendelea kubaki Benki kinara nchini.
Benki hiyo pia, imelitumia tukio hili la kihistoria kama sehemu ya kuwahamasisha wafanyakazi wake na Watazania kwa ujumla kushiriki utalii wa ndani ili kusaidia kukua kwa shughuli hiyo yenye fursa lukuki kibiashra na tija kiuchumi.
Timu hiyo ya NMB imetumia siku saba kupanda na kushuka Mlima Kilimanjaro wakianzia lango la Machame na kumalizia lango la Mweka, walipokelewa na wenzao kutoka ofisi ya Kanda ya Kaskazini pamoja na matawi ya Moshi.
Akizungumza wakati wa kuwapokea wafanyakazi hao kutoka mlimani, Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro Iman Kikoti ameeleza kuwa kitendo cha wafanyakazi wa NMB kupanda Mlima Kilimanjaro kinaimarisha nafasi ya benki hiyo kuendelea kuwa karibu na sekta ya utalii na mshirika wa kimkakati wa maendeleo ya taifa.
“Kwa sasa mchango wa utalii bado ni mdogo kwa hiyo uamuzi wa NMB kusaidia kuuchangamsha ni jambo jema na la kimaendeleo linalopaswa kuungwa mkono na wadau wote wa sekta binafsi,” amebainisha.
Mwezi wa Huduma kwa Wateja, unaadhimishwa duniani kote kila mwezi Oktoba.