Home AJIRA Waajiri watakiwa kuzingatia mishahara mipya

Waajiri watakiwa kuzingatia mishahara mipya

0 comment 228 views

Makamu wa Rais wa Tanzania Dk Phillip Mpango amewataka waajiri wa sekta binafsi kuanza kulipa mishahara mipya kama ilivyoagizwa na Serikali kuanzia Januari mwakani.

Viwango hivyo vya mishahara mipya, vilitangazwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi na Ajira na wenye ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako kwenye Gazeti la Serikali (GN) namba 697 la Novemba 25.

Katika viwango hivyo vipya, mfanyakazi anayefanya kazi katika migahawa, nyumba za kulala wageni na baa atalipwa kima cha chini cha Sh 150,000 kwa mwezi, hoteli za kati Sh 180,000 na hoteli za kitalii atalipwa Sh 300,000.

Mfanyakazi wa kazi za ndani ambaye haishi katika kaya ya mwajiri atalipwa Sh 120,000, huku wale wasoishi kw mwajiri watalipwa Sh 60,000 kwa mwezi, huku wafanyakazi wa kazi za ndani walioajiriwa na Wanadiplomasia na wafanyabiashara wakubwa wakilipwa kima cha chini cha Sh 250,000.

Katika hoteli kubwa za kitalii, mfanyakazi atalipwa kima cha chini Sh 300,000, hoteli za kati Sh 180,000, huku katika makampuni makubwa na kimataifa huduma ya ulinzi wakilipwa Sh 222,000 na makampuni madogo wakilipwa Sh 148,000.

Kwa wale wanaofanya kazi kwenye huduma za mawasiliano watalipwa kima cha chini cha Sh 500,000, wakati wafanyakazi wa huduma za utangazaji na vyombo vya habari, posta na usafirishaji vifurushi watalipwa kima cha chini Sh 225,000.

Katika sekta ya Nishati makampuni ya kimataifa watalipwa Sh 592,000 na makampuni madogo Sh 225,000, wakati katika sekta ya usafirishaji, wanaofanya katika huduma za usafiri wa anga watalipwa Sh 390,000.

Wafanyakazi wa kutoa huduma za utoaji mizigo na usambazaji watalipwa kima cha chini cha mshahara Sh 360,000 na wale wanaofanya katika huduma za usafiri nchi kavu watalipwa Sh 300,000.

Kwa upande wa makandarasi, makandarasi daraja la pili hadi la nne watalipwa kima cha chini Sh 360,000 huku daraja la tano hadi la saba wakilipwa kima cha chini ya mshahara cha Sh 320,000.

Huduma za shule binafsi kuanzia shule za awali, msingi na sekondari watalipwa kima cha chini cha Sh 207,000, huku katika sekta ya biashara na viwanda wakilipwa Sh 150,000 na Taasisi za fedha wakilipwa Sh 592,000 kwa mwezi.

Katika sekta ya madini, wenye leseni za uchimbaji na utafutaji madini wao kima cha chini cha mshahara kitakuwa Sh 500,000, huku wenye leseni za wachimbaji wadogo kikiwa Sh 300,000 na wenye leseni za wafanyabiashara ni Sh 450,000.

Taarifa ya Prof Ndalichako inabainisha kuwa sekta ya uvuvi na huduma za baharini kima cha chini ni Sh 238,000 na sekta nyingine zote ambazo hazijaainishwa katika tangazo hilo la Serikali, watalipwa mshahara wa Sh 150,000.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter