Home VIWANDANISHATI EU yatoa ruzuku 9bn kwa ajili ya mradi wa Nishati Safi Tanzania

EU yatoa ruzuku 9bn kwa ajili ya mradi wa Nishati Safi Tanzania

0 comment 265 views

Inakadiriwa Watanzania zaidi ya asilimia 80 wanatumia vyanzo vya nishati ya kupikia  ambavyo si salama na vyenye madhara ya kiafya, kiuchumi na kimazingira.

Tanzania imelenga kuboresha matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kutokana na umuhimu wa afya za Watanzania na Mazingira.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga akimuwakilisha Mgeni rasmi Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko, wakati wa kukabidhi hundi za takribani Tsh Bilioni tisa fedha za ruzuku zinazofadhiliwa na Nchi za Umoja wa Ulaya (EU).

Fedha hizo ni kupitia mfuko wa *CookFund* kwa wajasiriamali 44 wanaojihusisha na Mradi wa Nishati Safi ya Kupikia.

Ameeleza kuwa jitihada zinazofanyika zitasaidia kupunguza utegemezi wa Nishati zisizo safi na kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amehimiza kuwa uwepo wa programu endelevu za matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia zinalenga kusaidia Wananchi na kujikwamua katika hali za kiuchumi.

“Kwa kweli kwa niaba ya Wizara tunapenda kuwapongeza EU kwa mradi huu kabambe wa kuboresha na kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi ya kupikia, lakini vilevile mradi ambao unachagiza maendeleo katika Sekta ya Nishati nchini,” amesema Kapinga.

Aidha, ameongeza kuwa programu hiyo ni muhimu kwa Wizara na washirika kwa kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Wizara ya Fedha ambao kwa pamoja wameendelea kuboresha mnyororo wa thamani kutokana na umuhimu wa Nishati safi ya kupikia kwa ustawi wa Taifa.

Mkuu wa EU Cèdric Merel amesema, suala la Nishati safi ya kupikia lisichukuliwe kuwa ni la anasa na kwamba hitaji hilo lifikie kila kaya bila kujali hali ya kipato kwani inasaidia kuokoa muda, ni rahisi kutumia na inalinda mazingira.

Maono ya Serikali ni kuhakikisha inafikia lengo lake la asilimia 80 ya Watanzania kutumia Nishati Safi ya kupikia mpaka ifikapo mwaka 2033, nishati hii safi ya kupikia pia ipatikane kwa urahisi, na kwa ufanisi na kwa gharama nafuu.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter