Ofisa Uhusiano wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Malik Munisi amedhibitisha kuwa kumekuwa na mchakato wa kiwanda cha saruji cha Dangote kilichopo Mtwara kubadilisha mfumo wake wa nishati na kuanza kutumia gesi asilia.
Kiwanda hicho ambacho kimekuwa kikitumia mafuta ya dizeli kuendesha shughuli zake kimekuwa kikishirikiana na TPDC katika zoezi zima la ubadilishaji wa mitambo ambapo inatarajiwa kuwa, gharama ya sarufi itashuka mara baada ya kiwanda hicho kuanza kutumia gesi asilia kutokana na gharama za uzalishaji kupungua.
Tayari awamu ya kwanza ya mabadiliko hayo ambayo yametekelezwa na TPDC yameshakamilika ambapo kiwanda hicho kitaweza kutumia futi milioni nane za ujazo wa gesi asilia kuzalisha umeme wa kila siku. Awamu hiyo pekee imegharimu takribani Dola 915,953.59 za Marekani.