Suala la ugumu wa ajira hapa nchini wa halihitaji ufafanuzi kwani kila mmoja bila shaka alipitia au anapitia changamoto zake katika hili. Upatikanaji wa ajira umeendelea kuwa mgumu huku mamia ya vijana wakihitimu elimu ya juu kila mwaka. Ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuajiriwa, na kujitayarisha vya kutosha ili kuwavutia zaidi waajiri na kuwaonyesha tangu mwanzo kuwa mchango wako katika taasisi, kampuni au shirika lao utaongeza ufanisi. Zinazofuata ni baadhi ya mbinu ambazo unaweza kutumia kujihakikishia unafanya vizuri katika mahojiano ya kazi.
Kwanza kabisa unapaswa kufanya maandalizi. Baada ya kuomba kazi, ni vizuri kama utafanya utafiti wako ili kufahamu nini waajiri wako wanafanya. Hakikisha unazo taarifa zote za awali kuhusu kampuni husika na kile wanachofanya. Tayarisha nyaraka zako muhimu na jitahidi usizisahau siku ya mahojiano. Kama unao ushahidi unaoonekana wa kazi ulizowahi kufanya mfano nyaraka, picha au hata mradi endelevu, beba nyaraka hizo siku ya mahojiano.
Usikurupuke, jitayarishe kabla ya wakati. Andaa mahitaji yako yote kama vile nguo, nyaraka, fahamu itachukua muda gani kufika ofisini ili usichelewe na vilevile hakikisha unapumzika kabla ya mahojiano hayo. Uchovu sio kitu ambacho kinafichika hivyo hakikisha unapumzika vya kutosha na kujiandaa vyema kabla ya siku. Haitakuwa vizuri kama ukifika kwenye mahojiano ukiwa umechelewa au muonekano wako ukiwa sio nadhifu. Mbali na ujuzi na elimu yako, muonekano wako pia utakuweka katika nafasi nzuri ya kuajiriwa.
Ukiwa katika mahojiano jitahidi sana kuwa mtulivu. Usilazimishe kuwa mjuaji wa kila kitu. Sikiliza maswali unayoulizwa kwa umakini kwani toa jibu la moja kwa moja. Epuka majibu marefu sana na fanya majibu yako kuwa mafupi na yaliyojitosheleza. Andaa maswali utakayowauliza waajiri pembeni na tumia nafasi hiyo ya mahojiano kuonyesha kile unachokijua ili kuwashawishi wakuajiri wewe na sio waombaji wengine. Pia onyesha ufahamu na uelewa wa kile kinachofanywa na kampuni ili kuwadhihirishia kuwa umefanya utafiti wako mwenyewe na umejiandaa vyema kabla ya kufika mahali hapo. Usionyeshe uoga wa aina yoyote hata kama unaogopa.
Wahitimu wamekuwa wengi sana mitaani hivyo soko la ajira limezidi kuwa gumu. Kama vijana haipaswi kukata tamaa katika hili. Ukipata nafasi ya kuchaguliwa kwa ajili ya mahojiano, tumia nafasi hiyo kuonyesha kile unachnacho na kile waajiri watakachofaidika ikitokea umeajiriwa. Kuwa makini na majibu unayotoa, jiandae vyema, zingatia muda na mwisho kabisa jiamini kama unaweza. Ikitokea unakosa nafasi moja usikate tamaa, jaribu tena kwa moyo huo huo na tumia uzoefu wako kufanya vizuri zaidi katika mahojiano mengine.