Rais John Magufuli amesema utendaji kazi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) sio wa kuridhisha. Rais Magufuli ameeleza hayo katika hafla ya uzinduzi wa awamu ya pili ya Programu ya Kuendeleza Kilimo (ASDP II) na kuongeza kuwa mwaka 2017, serikali ilitoa mtaji wa Sh. 60 bilioni kwa TADB na bado benki hiyo ilichukua mkopo wa zaidi ya Sh. 207.05 bilioni kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB). Licha ya hayo, Rais Magufuli amesema benki hiyo imekuwa ikisuasua katika utoaji mikopo kwa wakulima na badala yake, wamekuwa wakifanya biashara na benki nyingine.
Rais Magufuli amedai kuwa serikali inakopa ili kuwezesha wakulima kupata mikopo lakini benki hiyo ya kilimo imekuwa ikichukua fedha hizo na kuzitumia kufanya biashara na taasisi nyingine hali ambayo imepelekea wakulima kuendelea kupata wakati mgumu.