Benki ya CRDB imeiokoa Benki ya Wananchi ya Tandahimba (Tanecu) ili isifungwe kwa kuipatia mtaji wa Sh. 3.2 bllioni ili iweze kujiendeshe kwa ufanisi zaidi.
Kiasi hicho cha fedha kimetolewa ili kutekeleza agizo la Benki kuu ya Tanzania (BoT) linalotaka benki za wananchi kuwa na mtaji unaoanzia Shilingi bilioni 2 na zile za taifa kuwa na mtaji kuanzia Sh. 15 bilioni.
Fedha hizo zitakabidhiwa ndani ya kipindi cha miaka miwili baada ya kufanyika kwa makubaliano na utiaji saini chini ya Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo Dk. Charles Kimei ambaye alisisitiza lengo la msaada huo ni kuhakikisha benki hiyo ya wananchi haifungwi bali na itaendelea kutoa huduma kwa wananchi.
Mwaka 2017 CRDB ilijitolea timu ya menejimenti kwenda kuisaidia benki hiyo katika uendeshaji kama moja ya mikakati yao katika kuwafikisha huduma kwa wananchi.
Benki ya wananchi wa Tandahimba ilianzishwa mwaka 2008 kwa mtaji mdogo wa Sh. 500 milioni ambao uliishia kwa kusimika mifumo ya kibenki na kwa kipindi cha miaka saba tangu kuanzishwa wamepata hasara inayokadiriwa kufikia kiasi cha Sh. 1.5 bilioni.