Home VIWANDA Tanzania ya viwanda ianze na watanzania wenyewe

Tanzania ya viwanda ianze na watanzania wenyewe

0 comment 113 views

Kuwekeza katika viwanda kama sera kuu ya na ya serikali iliyopo madarakani inayoongozwa na ilani ya Chama cha mapinduzi “Tanzania ya viwanda”. Sera ya Tanzania ya viwanda imekuwa ikitekelezwa kwa njia tofauti tofauti ikiwemo kuendeleza viwanda vilivyopo kwa sasa, kufufua vile vilivyokuwa vimekufa au vimeharibika mitambo yake, kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda, kupanua wigo mkubwa wa viwanda vilivyokuwa vikizalisha kwa kiasi kidogo na hatimaye kuzalisha kwa wingi, sambamba na ujenzi wa viwanda vipya kabisa.

Ni dhahiri kuwa, suala la kuwekeza katika viwanda linahitaji kugharimiwa kwa kiasi kikubwa kifedha lakini pia kuwekeza katika muda kwani inachukua muda sana hadi nchi kufikia na kutimiza matakwa yake hasa katika kutekeleza sera mbalimbali zinazoanzishwa na serikali, katika kiwango cha kuridhisha.

Ni mara kadhaa tumesikia neno mapinduzi ya viwanda (Industrial Revolution). Neno hili si geni sana kwa walio wengi. Mapinduzi ya viwanda kwa mara ya kwanza yalianzia mwaka 1760-1840 nchini Uingereza ikiwa ni matokeo ya kuwepo kwa uzalishaji mwingi uliopitiliza kiasi cha kushuka kwa bei ya bidhaa lakini pia kukosa walaji au watumiaji.

Mapinduzi ya viwanda hayakuja tu kutokana na viwanda vikubwa bali mapinduzi haya yalianzia nyumbani. Hicho kilikuwa ni kipindi ambacho asilimia 80 ya watu nchini Uingereza walijihusisha na uzalishaji kupitia viwanda ikiwemo viwanda vya kushona nguo, kufua chuma, kuchakata malighafi na kadhalika.

Dhana na sera ya Tanzania ya Viwanda haipaswi kuchukuliwa kwa mapana tusiyoyaweza, bali tunatakiwa kuifikiria Tanzania ya Viwanda kulingana na uwezo wetu na hali zetu za maisha. Sio kwamba Tanzania haiwezi kuwa na viwanda vya magari, hapana, bali kinachozungumziwa hapa ni wewe mtanzania umejiandaa vipi kuelekea Tanzania mpya ya Viwanda?

Kadri siku zinavyozidi kwenda mbele tumekuwa tukishuhudia ongezeko la mashine za kutengenezea juisi ya miwa, matunda, kuchomelea vyuma, kupaka rangi, mashine za kuvunia na kutwangia mahindi tena zikiwa zinamilikiwa na watu kadhaa sio mjini tu bali hata vijijini.

Kama kuna watu waliweza kuzalisha majumbani kwao hadi bidhaa zao zikakosa wanunuaji ni dhahiri kuwa hawa watu walikuwa wamedhamiria kuhakikisha viwanda vinakuwa nguzo kuu ya uzalishaji katika nchi. Haikuchukua muda mapinduzi ya viwanda yaliyoanza Uingereza yaliweza pia kuenea katika nchi mbalimbali barani Ulaya.

Sera hii ya Tanzania ya viwanda isichukuliwe kama jukumu la serikali tu bali mimi na wewe tunaweza pia kuonyesha kuwa tumedhamiria kuipeleka Tanzania kuwa nchi ya viwanda. Huko nyuma kidogo, tulizoea kuona bisi za kukaangwa zikitoka viwandani na kusambazwa madukani. Sasa hivi bisi (popcorn) hazitoki viwandani bali zinatembezwa mtaani huku zikiwa zinazalishwa papo hapo.

Ukitaka kuhakikisha jinsi biashara hii ilivyowapatia ajira vijana  wengi tembelea stendi ya daladala ya Makumbusho jijini Dar es Salaam. Viwanda vinaanzia hapo sio lazima kiletwe kiwanda cha kutengeneza magari. Mapinduzi ya viwanda sio Ulaya tu bali hata Tanzania inawezekana kikubwa ni kuweka nia katika kuhakikisha Tanzania na watanzania wote kwa ujumla wanatumia teknolojia katika kuhakikisha wanafikia uchumi wa kati sambamba na kuitekeleza sera ya Tanzania ya viwanda.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter