Kufuatia mgomo wa minada ya siku mbili, Rais wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli ametoa msimamo wa serikali na kueleza kuwa anaunga mkono maamuzi yaliyofanywa na wakulima na kwamba yupo nao bega kwa bega huku akisisitiza kuwa, bei ya korosho isiwe chini ya Sh.3,000 kwa kilo moja. Rais Magufuli amesema hayo jana (Oktoba 28, 2018) alipokutana na wadau na wanunuzi mbalimbali wa korosho katika kikao kilichofanyika jijini Dar es salaam. Mgomo huo umetokana na wakulima wa zao la korosho mikoani Lindi na Mtwara kugoma kuuza zao hilo wakidai bei imeshuka ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita wakati gharama za uzalishaji zikiendelea kupanda.
“Nawataka wafanyabiashara muelewe kuwa, hakuna korosho itakayouzwa chini ya Sh. 3,000. Kama hamtanunua, mniambie. Serikali tunaunga mkono wakulima kukataa bei za korosho. Ndio maana kiongozi wa Bodi ya Korosho alipowatisha wakulima kuwa lazima wakubali, tumemuondoa, na hatorudi huko”. Amesema Rais Magufuli.
Viongozi wengine walioshiriki kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere ni pamoja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba na watendaji wengine wa serikali.