Benki ya China Dasheng Bank Limited imeanza rasmi kutoa huduma za kibenki jijini Dar es Salaam, ikiwa na mtaji wa kuanzia wa Sh. 92 bilioni, sawa na Dola za kimarekani milioni 40. Akizungumza katika uzinduzi wa benki hiyo mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya benki hiyo, Yu Jiaqin amesema China Dasheng ni benki ya kibiashara inayomilikiwa na makampuni sita ya serikali ya China yakishirikiana na makampuni binafsi. Jiaqin amesema benki hiyo inalenga kutoa huduma kwa makampuni makubwa ya China yenye miradi mbalimbali hapa nchini, lakini pia kwa watanzania wanaofanya biashara na China, huku makundi yote ya watu wenye kipato cha chini, cha kati na cha juu yakizingatiwa.
“Tutatoa huduma za bidhaa zote za kawaida za kibenki kama vile akaunti za akiba, akaunti za kudumu na za muda maalum, mikopo ya muda mfupi na muda mrefu na mikopo hii itatolewa kwa Shilingi za kitanzania pamoja na fedha za kigeni.” Ameeleza Mwenyekiti huyo wa bodi.
Kwa upande wake, Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo, Nunu Saghaf ameishukuru Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuwapatia leseni ya kufanya biashara na kuahidi kuisaidia serikali kutimiza azma ya uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.
Naye Balozi wa China hapa nchini Wang Ke amesema kufunguliwa kwa benki hiyo ni ishara ya ushirikiano wa muda mrefu baina ya China na Tanzania na benki hiyo itaboresha huduma za kifedha na hivyo kuwanufaisha wafanyabiashara kutoka pande zote.