Waziri wa Viwanda na Biashara Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali amesema baada ya serikali kufanya utafiti na kubaini kuwa eneo la Micheweni sio rafiki kwa kilimo cha miwa, serikali imefuta mpango wa kujenga kiwanda cha sukari katika kijiji hicho kufuatia jiografia ya ardhi katika eneo hilo kuwa ya mawe. Waziri huyo ametoa tamko hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Migombani na kueleza kuwa, serikali ina mpango wa kujenga kiwanda cha mafuta ya mkaratusi kijijini humo.
“Tumefanya utafiti na kuona kuwa ardhi ya Micheweni inakubali kwa miti ya mikaratusi, hivyo serikali hivi sasa inafanya utaratibu wa kuipanda kwa ajili ya kuzalisha mafuta ya mkaratusi”. Ameeleza Balozi Ali.
Waziri huyo amewaambia waandishi wa habari kuwa, Zanzibar imepata soko la mafuta hayo nchini China na hivi sasa, zoezi la kupanda mikaratusi eneo la Micheweni linaendelea. Balozi Ali amebainisha kuwa viwanda vina mchango mkubwa katika kutoa ajira hasa kwa vijana ambao wanakumbana na tatizo la kukosa ajira kwa kiasi kikubwa. Mbali na hayo, Waziri Ali ameweka wazi kuwa, Shirika la Biashara limeanzisha viwanda vidogo vya viungo na kutoa wito kwa vijana kulima mazao hayo kwa wingi kwani kuna soko la uhakika ndani na nje ya nchi.