Meneja Miradi kitengo cha Uzalishaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mhandisi Stephene Manda ametoa wito kwa wananchi kuwekeza katika viwanda na kuunga mkono harakati za serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli kufikia uchumi wa kati na wa viwanda kwani umeme hivi sasa ni wa uhakika. Mhandisi Manda amesema hayo wakati akielezea utekelezaji wa miradi ya umeme ya Kinyerezi I na Kinyerezi II jijini Dar es salaam.
“Mradi wa Kinyerezi namba II wa Megawati 240 umekamilika, kwa hivyo ombi letu kwa wote ambao wanaweza kuwekeza kwenye viwanda wawekeze kwani umeme wa uhakika na wa kutosha upo. Licha ya mradi huo wa Kinyerezi II mradi mwingine ni wa upanuzi wa Kinyerezi I unaozalisha megawati 150 ili ufikie Megawati 335 kwa kuongeza Megawati 185. Itakapofika Agosti 2019, jumla ya umeme utakaokuwa unatoka Kinyerezi pekee ni Megawati 575 kwa hivyo ni umeme wa kutosha, kama ni kulisha Dar es salaam, basi Dar es salaam nzima Kinyerezi inaweza kuibeba.”
Pamoja na hayo, Meneja huyo amesema kuwa TANESCO imejipanga vizuri na kuwataka wawekezaji waendelee kuwekeza katika sekta ya viwanda huku akisisitiza kuwa, lengo la kufikia uchumi wa viwanda linawezekana kwani umeme ni wa uhakika.