Mkuu wa wilaya ya Rombo, Agness Hokororo amewashauri wafanyabiashara wadogo wilayani humo waliopatiwa vitambulisho kujikita katika kufanya biashara halali na sio za magendo. Hokororo ametoa wito huo wakati akikabidhi vitambulisho zaidi ya 500 na kusema huwa, wafanyabiashara hao hivi sasa wanatambulika kwa mujibu wa Sheria hivyo hakuna sababu ya kukimbia.
Mkuu huyo wa wilaya ameeleza kuwa zipo changamoto za kuwepo kwa wafanyabiashara wasio waaminifu kupitisha bidhaa pasipo kufuata taratibu na Sheria kwa kuwa wilaya hiyo ipo mpakani mwa nchi jirani ya Kenya. Hokororo ameonya kuwa serikali haitalifumbia macho suala la biashara za magendo licha ya kuwa na kitambulisho.
“Wapo wafanyabiashara wanaodhani kuwa na kitambulisho hiki kunaondoa uwepo wa serikali kukamata bidhaa zinazoingizwa nchini kinyume na Sheria la hasha….pia wale wauza gongo kitambulisho hakihalalishi hilo. Tujitahidi kuzingatia taratibu za kisheria”. Amesema Mkuu huyo.
Kwa upande wake, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wilayani Rombo, Hermance Nghase amewasisitiza wafanyabishara hao kutunza kumbukumbu ili kufahamu mwenendo wa biashara zao.