Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amesema wapo katika hatua za mwisho za marekebisho ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290, ili kuimarisha na kuongeza usimamizi na ukusanyaji wa mapato ya ndani. Jafo ameeleza kuwa kufanya hivyo kutasaidia kuondoa changamoto za ukusanyaji mapato ya ndani kwa mamlaka hizo.
“Sheria hiyo imetumika kwa muda mrefu tangu 1982 hivyo, marekebisho hayo yanalenga kuweka uhalisia wa utendaji wa sasa katika namna bora zaidi ya usimamizi na ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa”. Amefafanua Jafo.
Pamoja na hayo, Waziri huyo ameeleza kuwa kwa muda wa nusu mwaka, halmashauri zimekuwa zikipata changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya wanunuzi kuchelewesha malipo wa ushuru na hivyo kusababisha makusanyo kuwa ya chini.
“Pia baadhi ya halmashauri kutegemea zaidi chanzo kimoja na kushindwa kukusanya kutoka kwenye chanzo hicho kunaweza kusababisha halmashauri hizo kushindwa kujiendesha”. Ameeleza Waziri huyo.
Aidha, Waziri Jafo amesema kuna mikakati mbalimbali iliyopo ili kutatua changamoto hizo huku akisisitiza kuwa, TAMISEMI itaendelea kusimamia halmashauri zote zinazosuasua kwa karibu katika suala la ukusanyaji mapato.