Tanzania imeanza utekelezaji wa mradi mkubwa wa kuunganisha umeme kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ambapo imeelezwa kuwa, baad ya mradi huo kukamilika, nchi itapata fursa ya kuuza nishati hiyo kwa nchi nyingine. Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari wilayani Monduli mkoani Arusha, Mratibu wa mradi huo Peter Kidagye amesema mradi huo mkubwa utagharimu Dola za Marekani 258.82 Milioni ( takribani Sh. 600 Bilioni za Tanzania) na umefadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Japan (JICA), Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB) pamoja na serikali.
Baada ya kukamilika, mradi huo unaofahamika kama Kenya-Tanzania Power Interconnector Project (KTPIP)/ZTK utaongeza usambazaji kwa mikoa ya kusini na kuimarisha biashara ya umeme kwa taasisi, utawezesha Tanzania na Kenya kupunguza gharama kubwa za umeme unaofuliwa kwa gesi na kutumia ule wa gharama nafuu wa maji.
Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi wa Miradi ya TANESCO, Emmanuel Manirabona amesema tayari vifaa kwa ajili ya mradi huo vimeshawasili na wakandarasi waendelea na kazi.