Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Jublet Mnyenye amesema takribani wananchi 40,000 wilayani humo wapo katika hatari ya kukosa majisafi endapo serikali haitachukua hatua stahiki kulinda miundombinu ya mifereji katika Bonde la Easi ambacho ndio chanzo cha maji kinachotumika wa wakazi wa wilaya hiyo.
Mnyenye amesema hayo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu na kueleza kuwa, changamoto ya miundombinu imepelekea kuwa na matatizo katika ugawaji maji.
“Katika Bonde lile la Easi kuna chanzo kimoja cha maji ya chemichemi, kuna shida sana ya utunzaji wa miundombinu, siombei lakini ikatokea bahati Mbaya kile chanzo kikafa hapa Karatu hatutaenea. Kuna watu nafikiri zaidi ya 40,000 wako pale wanategea chanzo kile na wakati huo huo lile bonde linatumiwa na wakulima kuzalisha zao ambao hata kwetu kama nchi linatuletea fedha za kigeni, linazalisha vitunguu ambavyo zaidi ya asilimia 80 vinapelekwa Kenya”. Ameeleza Mwenyekiti huyo na kuongeza kuwa:
“Tumeomba mambo mengi sana na tumeeleza shida nyingi sana, mimi ningesema basi angalau ule mradi mmoja wa kwa Tom, kwa kipindi hichi serikali ingetuangalia kwa jicho la pekee, ukikamilika utakuwa umepunguza shida kubwa ya maji”.