Rais wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli amesema kufuatia hatua madhubuti zilizochukuliwa na serikali ya awamu ya tano, taifa linakwenda katika muelekeo mzuri kutokana na kuimarishwa kwa uchumi na huduma mbalimbali za kijamii kama vile afya, elimu, maji, nishati pamoja na miundombinu ya usafiri.
Rais Magufuli amesema hayo wakati akizungumza na wananchi eneo la Zanaki wilayani Ilala ikiwa ni muda mfupi baada ya kutembelea kampuni ya Africa Media Group (AMGL) inayomiliki vituo vinne vya televisheni ikiwemo Channel Ten na vituo viwili vya redio ikiwemo Magic FM.
Aidha, Rais Magufuli amesema pamoja na mafanikio yote hayo, serikali itaendeleza jitihada za kupambana na dhuluma na vilevile matumizi mabaya ya rasilimali za taifa. Rais Magufuli pia ametoa wito kwa watanzania wote kuunga mkono serikali kwa kuhakikishia wanatanguliza maslahi ya taifa.