Kampuni ya mafuta ya Total Tanzania Limited, imezindua rasmi kiwanda chake cha vilainishi na kufanya kampuni hiyo ya mafuta kuwa pekee ya kimataifa hapa nchini kuzalisha vilainishi vyake yenyewe ambapo inatarajiwa kuwa, takribani tani 15,000 za vilainishi zitazalishwa kwa ajili ya soko la ndani huku ziada ikiuzwa nje ya nchi.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Joseph Kakunda amesema kiwanda hicho kilichopo eneo la viwanda la Chang’ombe Dar es salaam mbali na kutengeneza ajira kwa wananchi pia kitasaidia taifa kwa kiasi kikubwa.
“Endapo kiwanda hiki kisingejengwa, tungebaki na kiwanda kimoja cha vilainishi hapa nchini, hivyo kiwanda hicho kingezidiwa na kusababisha matokeo mabaya. Hivyo kiwanda hiki kitasaidia katika mambo mbalimbali. Vilainishi ni kitu muhimu na kila mtu anavitegemea, hivyo tunahitaji vilainishi vingi mara kwa mara”. Amesema Waziri Kakunda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Total Tanzania, Tarik Moufaddal amesema kampuni hiyo ya mafuta imekuwepo hapa nchini kwa zaidi ya miaka 50 na imekuwa ikiagiza vilainishi vyake kutoka nje ya nchi lakini kufuatia uwepo wa kiwanda hicho, kuanzia sasa vilainishi hivyo vinatengenezwa hapa nchini, ikiwa ni ishara ya kuunga mkono kwa vitendo jitihada za Rais Magufuli na serikali ya awamu ya tano katika ujenzi wa Tanzania ya viwanda.
“Kiwanda hiki licha ya kuchangia katika maendeleo ya taifa kiuchumi na kitekinolojia, pia kitatoa nafasi za ajira kwa watanzania”. Amesema Moufaddal.