Meneja wa Shirika la kuhudumia viwanda vidogo (SIDO) jijini Arusha, Nina Nchimbi ametoa wito kwa vijana kuwa wabunifu na kuanzisha teknolojia mpya nchini ili kuwasaidia wajasiriamali na vilevile kuchochea uzalishaji wa bidhaa. Nchimbi ameeleza kuwa, iwapo teknolojia hizo zitavumbuliwa, zitawasaidia wazalishaji wa viwanda vidogo na kuwanufaisha vijana hao na pato la taifa kwa ujumla.
Meneja huyo ameongeza kuwa, shirika hilo linawapa fursa kuanzisha teknolojia mpya nchini na hivyo kuwataka vijana hao kutotegemea teknolojia za nje kwani wanawanufaisha waliogundua teknolojia hizo na badala yake, wanaweza kutumia fursa hizo kunufaika.
“Ninachowaomba vijana wa Tanzania badilikeni kwa kujituma na kuwa wabunifu, ili kunufaika zaidi badala ya kutegemea vitu vilivyobuniwa na wenzenu nchi zingine” . Amesema Meneja huyo.
Kwa upande wake, Mratibu wa INFOY Laurent Sabuni amesema lengo la baraza hilo ni kuwakumbusha vijana kuwa fursa ni nyingi na kuwataka kuzichangamkia ili waweze kuchangia katika uchumi wa taifa.
“Nchi yoyote haiwezi kuendelea kama hakuna ubunifu wa teknolojia na bidhaa mbalimbali ambazo nchi inaweza kuviuza katika masoko ya nje na kuleta faida”. Amesema Mratibu huyo.