Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewakaribisha wawekezaji kutoka nchini India, Misri na Falme za Kiarabu kuwekeza hapa nchini na kuwahakikishia kuwa, serikali itawapa ushirikiano wa kutosha. Majaliwa amesema hayo wakati alipokutana na mabalozi wa Misri, India na Falme za Kiarabu wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania kwa nyakati tofauti.
Waziri Majaliwa amesema serikali imepanga kuendeleza sekta ya viwanda nchini ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Aidha, ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wafanyabiashara kuja kuwekeza hapa nchini. Amesema kuwa, Ofisi yake kupitia Waziri mwenye dhamana ya uwekezaji, Angellah Kairuki ipo tayari kuwasikiliza na kuwasaidia wawekezaji wote.
“Tanzania iko tayari wakati wote kutoa ushirikiano ili kuhakikisha wawekezaji watakaojitokeza kuwekeza nchini wanafanikiwa ili mataifa yote yaweze kufaidika.”Amesema Waziri Mkuu
Kwa upande wa mabalozi hao, wameishukuru serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mzuri na nchi zao na kuhakikisha kuwa watauendeleza. Pia wameeleza nia yao ya kushirikiana na Tanzania kuhakikisha mpango wa serikali kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda unafanikiwa.