Baada ya kukamilika ujenzi wa miundombinu ya mradi wa gesi asilia, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeanza kuunganisha gesi hiyo ambapo kwa awamu ya sasa wanategemea kuunganisha katika nyumba zaidi ya 100.
Hadi sasa wameshaingiza gesi hiyo kwenye nyumba 24, huku Migahawa minne ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ikiwa kwenye idadi ya nyumba hizo 100 zitakazowekewa gesi hiyo.
Msimamizi wa Usambazaji Gesi Majumbani wa Shirika hilo Ismail Naleja, amesema kabla ya kuanza kuunganisha rasmi gesi hiyo kwenye nyumba za watu walifanya majaribio katika nyumba 72 mikocheni na majaribio hayo yalivyokwenda vizuri wakaona hakuna sababu ya kutotekeleza mradi huo.
Hata hivyo, ameeleza kuwa wameanza kuunganisha gesi hiyo Mikocheni kwasababu miundombinu inaruhusu kwani walifanya majaribio huko. Hivyo ametaja maeneo ambayo yatasambaziwa mradi huo kuwa ni Mlalakua, Chuo Kikuu,Mikocheni kwenye Migahawa minne ya Hosteli ya Magufuli, na Chuo kishiriki cha Uhandisi na tekinolojia (CoET).
Kutokana na gharama ya kuunganisha gesi hiyo kuwa shilingi milioni moja hadi milioni 1.8 wanategemea kufanya mabadiliko hapo baadae ili watu wengi wahamasike kuitumia. Pia amesema wateja wa gesi hiyo watarajie kulipa shilingi 25,000 ambayo ni nusu ya shilingi 50,000 ambayo hulipwa kwa ajili ya gesi.