Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIUJASIRIAMALI Jiajiri kwa kufanya unachopenda

Jiajiri kwa kufanya unachopenda

0 comment 179 views

Umewahi kufikiria kuwa kile unachopenda kinaweza kukuingizia kipato na kugeuka biashara? Asilimia kubwa ya wajasiriamali hupata mafanikio kutokana na kufanya kitu ambacho wanakipenda. Ukiongeza ubunifu katika kile unachofurahia kufanya, unaweza kutoa huduma hiyo kwa watu wengine na kuanzisha biashara tena kwa mtaji mdogo tu. Hapo chini ni baadhi ya mbinu unazoweka kufuata ili kuanzisha biashara yako.

  1. Tathmini kile unachopenda- Kabla ya kufanya maamuzi yoyote jiulize je kitu hicho kina uwezo na kukuingizia kipato? Watu wengine watafurahia huduma au bidhaa hiyo? Kuna soko la uhakika? Fanya utafiti ili kuona kama biashara hiyo itakufisha mbali na tambua nani hasa ni soko lako.
  2. Fanya majaribio- Badala ya kuwekeza tu, ni vizuri kufanyia majaribio kile unachotaka kufanya ili kuona jamii inayokuzunguka itakavyopokea huduma yako. Kabla ya kuacha ajira ya uhakika, fanya majaribio ili kuona uwezo halisi wa biashara hiyo.
  3. Uza kwa ndugu, jamaa na marafiki- Kundi hili ndio wateja wako wakubwa kwani tayari wanakufahamu hivyo ni soko zuri la kuanzia. Wafahamishe marafiki zako kuhusu huduma unayotoa, jitangaze kupitia mitandao ya kijamii na tambulisha biashara yako kwao. Wageuze watu hao kuwa wateja wako.
  4. Maarifa ya biashara- Pamoja na kupenda unachotaka kufanya, unapaswa kuwa na ujuzi na maarifa ya sekta ya biashara kwa ujumla ili kufanikiwa. Unaweza kusoma na kuelewa mazingia ya biashara kwenye tovuti mbalimbali au kwa kutembelea semina ambazo huandaliwa kuelimisha wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo. Biashara yenye mafanikio huhitaji maarifa na sio tu upendo.
  5. Fuatilia taratibu za Sheria- Kila biashara huwa na kanuni na taratibu zake kwa mujibu wa Sheria. Anza kufuatilia ili kujua taratibu gani za kisheria unapaswa kuzifuata. Hakikisha biashara unayoanzisha inaheshimu kanuni hizo.
  6. Kuwa tofauti na wengine- Bila shaka hiyo biashara unayoifikiria tayari ipo sokoni. Ili kuvutia wateja na kufanikiwa, kuwa tofauti na wale ambao tayari wapo. Kuwa mbunifu na wape sababu wateja kufuata huduma kwako na sio sehemu nyingine. Fanya mabadiliko katika utoaji huduma na jitofautishe na wale wanaofanya huduma kama hiyo.

Katika ulimwengu wa sasa, kama kijana hupaswi kutegemea ajira pekee. Siku hadi siku, soko hilo linazidi kuwa gumu na ajira zinazotolewa ni chache. Ni muda wa kufikiria nje ya boksi na kuwa mbunifu ili kujiingizia kipato. kuna fursa mbalimbali katika jamii zetu, muda wa kuzitumia umefika.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter