Na Mwandishi wetu
Rais wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Abdel Fattah Al Sisi anatarajia kuwasili nchini leo kwa ziara ya kitaifa baada ya mwaliko wa Rais John Pombe Magufuli. Lengo kubwa la ziara hii ni kuimarisha na kukuza mahusiano mazuri ya kidiplomasia, kiuchumi na kijamii yaliyopo kati ya nchi hizi mbili.
Katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ziara hii itatoa fursa kwa wakuu hawa wa nchi kubadlishana mawazo kuhusiana na masuala mabalimbali yanayoendelea katika nchi hizi mbili.
Kwenye taarifa hiyo pia, Tanzania na Misri zimeelezwa kuwa na mahusiano mazuri kwa muda mrefu sasa na kwamba mahusiano haya yametokana na ushirikiano wa karibu waliokuwa nao Hayati Baba wa Taifa wa Tanzania Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Muasisi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Gamal Abdel Nasser.
Tanzania na Misri zimekuwa zikishirikiana katika masuala mbalimbali yakiwemo yale ya kiuchumi, ulinzi na usalama pamoja na masuala ya kijamii. Kwa takwimu za mwaka 2016, nchi ya Misri ilishika nafasi ya pili kwenye nchi zenye uchumi mkubwa barani Afrika.