Baada ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya kutembelea ofisi zote za Halmashauri wilayani humo na kutoa vitambulisho kwa wakuu wa Idara, DC huyo amewafuata mnadani wafanyabiashara wadogo zaidi ya 500 ambao ni wafugaji kutoka jamii ya kimasai na kugawa vitambulisho hivyo mwenyewe.
“Sasa sikilizeni nyie wafugaji, Mheshimiwa Rais Magufuli amechapisha vitambulisho hivi kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara wadogo kutobugudhiwa. Leo nimekuja hapa nataka kila mtu awe nacho na kinatolewa kwa bei ya Sh. 20,000 tu”. Amesema Ole Sabaya.
Mwaka jana wakati wa mkutano wake na watendaji kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na wakuu wote wa mikoa hapa nchini, Rais Magufuli alitangaza uamuzi wake wa kugawa vitambulisho maalum kwa ajili ya kuwatambua wafanyabiashara wadogo ambao mapato yako kwa mwaka ni chini ya Sh. 4 milioni na kuwawezesha kufanya shughuli zao bila usumbufu wa aina yoyote.
Katika ziara zake hivi karibuni, Rais Magufuli ameendelea kuhamasisha ugawaji wa vitambulisho hivyo kwa wafanyabiashara na kuwaonya watendaji wa serikali ambao wamekuwa wakitoza fedha nyingi zaidi kutoa vitambulisho hivyo.