Home BIASHARAUWEKEZAJI Magufuli, atoa siku saba taratibu za uwekezaji kukamilishwa

Magufuli, atoa siku saba taratibu za uwekezaji kukamilishwa

0 comment 117 views

Rais, John Pombe Magufuli, amefanya mazungumzo na Kampuni ya Sugar Investment Trust (SIT) ya Mauritius, na kutoa agizo kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya  Makazi na Wizara ya Viwanda na Biashara kukamilisha taratibu za uwekezaji kwa Kampuni hiyo ndani ya siku saba.

Magufuli, amefanya maamuzi hayo jana baada ya kubaini kuwa kampuni hiyo imekuwa ikicheleweshwa kuwekeza katika  biashara ya Sukari toka mwaka 2017.

Mwenyekiti wa kampuni hiyo, Gansam Boodram, amemueleza Magufuli kuwa kampuni hiyo ipo tayari kulima ekari 25,000 za mashamba ya miwa, ambapo wataweza kuzalisha sukari tani 125,000, kutoa ajira za kudumu 3000 na ajira za muda 5000.

Taarifa kutoka Ikulu imeeleza kuwa Rais Magufuli, ameagiza uchambuzi wa haraka ufanywe katika Bonde la mto Rufiji Mkoani Pwani,  eneo la shamba la Mkulanzi lililopo Morogoro, na eneo la Kibondo Kigoma, ili SIT wawekeze.

“Uzalishaji huo utamaliza upungufu wa tani zaidi ya 100,000 ambazo kwa sasa zinaagizwa kutoka nje ya nchi’ ameeleza Rais huyo.

Mbali na hayo, Rais, ametoa agizo kwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Edward Mhede, kushughulikia makubaliano ya ushirikiano kwenye uvuvi baina ya Tanzania na Mauritius ambayo nayo hayajafanyiwa kazi toka mwaka 2017.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter