Wakati akifungua Mhadhara wa Umma ambao umeendeshwa na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Spika wa Bunge, Job Ndungai ametaja hatua nne kwaajili ya maendeleo ya biashara zinazotokana na mazao ya kilimo na viwanda vinavyotokana na usindikaji wa mazao hayo.
Mhadhara huo ulilenga kujadili mwelekeo wa upatikanaji wa chakula, kukuza mnyororo wa thamani wa bidhaa zinzotokana na kilimo duniani, huku ukienda sambamba na uzinduzi wa shahada ya Sayansi na Uchumi na fedha itakayotolewa na chuo hicho.
Mheshimiwa Ndungai, ametaja sababu hizo kuwa ni ulazima wa serikali kuwawekea mazingira mazuri na sera wafanyabiashara wadogo na wa kati pamoja na viwanda vinavyosindika mazao ya kilimo ili viweze kukua na kustawi.
Hatua nyingine amesema ni, kuwapa msaada wazalishaji wadogo ili waweze kushindana na soko la ndani, kikanda, na kimataifa kwa kuwapa mafunzo ambayo yatasaidia kuboresha stadi zao za usimamizi katika shughuli zao. Ameshauri chuo hicho kuwezesha mafunzo hayo kwa kutoa elimu na stadi za biashara katika suala zima la kilimo.
Pia ametaja hatua nyingine kuwa ni upatikanaji dhaifu wa huduma za kifedha kwa mda mrefu jambo ambalo limedumaza maendeleo vijijini. Ndungai ametaja hatua ya nne kuwa ni umuhimu wa kufanya uwekezaji katika utafiti wa kilimo ili kuibua tekinolojia mpya katika upande wa kilimo ambazo zitasaidia changamoto za mabadiliko ya nchi.
Naye, Mkuu wa Chuo cha IFM, Tadeo Satta amesema katika hatua ya kuisaidia serikali kukuza sekta ya viwanda na uchumi, chuo hicho kimeona kuna umuhimu wa kuandaa mihadhara kama hiyo ili kutoa elimu kwa umma.