Taarifa ya pamoja iliyotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) imeeleza kuwa kufuatia majadiliano yaliyofanyika hivi karibuni, taasisi hizo zimekubali kushirikiana katika maeneo mapya ya kilimo ili kuendeleza sekta hiyo.
“Ubunifu ni muhimu sana katika kukifanya kilimo kuwa cha kisasa nchini, TADB, WFP wanafanya kazi ya kuhakikisha kwamba nyanja hii inapewa kipaumbele kwenye kilimo hapa nchini kwa namna mbalimbali”. Imesoma taarifa hiyo.
Pia katika taarifa hiyo, imeelezwa kuwa hadi sasa taasisi hizo mbili zinashirikiana kutekeleza mradi wa ‘shambani mpaka sokoni’ ambao unafahamika kama Farm to Market Alliance (FTMA) ambapo vikundi 8 vyenye wanachama 867 wanaolima heka 2,789 katika mkoa wa Ruvuma na Rukwa vimeshapata mikopo inayofika Sh. 750 milioni kutoka katika benki ya TADB.
Aidha, taarifa imesema kuwa benki hiyo imejikita katika masuala ya fedha wakati WFP imejikita katika ubunifu, huku wakiwa na makubaliano ya kutumia mbinu mbalimbali ili kukabiliana na upotevu wa mazao, lengo likiwa ni kuongeza mavuno nchini.
“Benki inataka kuhakikisha kwamba inafanya kazi kufanikisha uanzishwaji wa miradi ya kilimo yenye tija na kuongeza huduma za kifedha ili uwepo wake uwe na matunda kwa wananchi wote”. Imeelezwa.
Mbali na hayo, TADB imepanga kufadhili angalau miradi 20 ya umwagiliaji na miradi 10 ya utunzaji wa mazingira ili kutekeleza mpango wa kuendeleza kilimo (ASDP II).