Mkurugenzi wa shughuli za kitakwimu kutoka Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), Irenius Ruyobya ametangaza kuwa mfumuko wa bei wa taifa kwa mwaka ulioishia Aprili umeongezeka na kufikia asilimia 3.2. Ruyobya ameeleza hayo jijini Dodoma na kuongeza kuwa, hali hiyo imetokana na kupanda kwa bei ya bidhaa za chakula na zisizo za chakula ikilinganishwa na bei za Aprili mwaka jana.
Baadhi ya bidhaa zilizochangia mfumuko wa bei kupanda ni pamoja na mafuta ya kupikia (9.9%), samaki (12.2%), mihogo mibichi (8.5%), maharage (13.3%) na matunda (12.6%).
“Kwa upande wa bidhaa zisizokuwa za chakulazilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa mwezi Aprili ni pamoja na mavazi (3.8%), huduma za malazi kwenye nyumba za wageni (6.1%), gesi ya kupikia (2.6%), mkaa (10.9%), gharama za kumuona daktari hospitali za binafsi (6.6%) na dizeli (8.5%)”. Amesema Mkurugenzi huyo.
Kwa upande wa vyakula na vinywaji baridi, Ruyobya amesema mfumuko wa bei umeongezea kutoka asilimia 0.1 ya mwaka ulioshia Machi 2019 hadi asilimia 0.9.
Akizungumzia hali ilivyo kwa baadhi ya nchi za ukanda wa Afrika Mashariki, Mkurugenzi huyo amesema mfumuko nchini Uganda umeongezeka kutoka asilimia 3.0 hadi asilimia 3.5. Kwa upande wa Kenya, mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Aprili 2019 umeongezeka hadi asilimia 6.58.