Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imetekeleza ahadi iliyotolewa Februari mwaka huu kwa kupeleka umeme katika migodi ya wachimbaji wadogo wa madini katika kijiji cha Nyakafuru kilichopo wilaya ya Mbogwe.
Inaelezwa kuwa, wachimbaji hao walikuwa wanatumia mafuta kufanya shughuli zao ikiwemo kuendesha mitambo ya kuchenjua madini, hali iliyowapelekea kutumia gharama inayofikia milioni 3 kwa mwezi kwa ajili ya kununua mafuta, jambo lililomfanya Waziri huyo kuwaahidi umeme ili kurahisisha shughuli zao.
“Serikali inatekeleza ahadi zake badala ya kupiga maneno, hivyo tumeleta umeme hapa si kwa ajili ya kuwasha taa tu, bali umeme huu utawawezesha kuchimba kwa tija, serikali inataka mchimbe kwa faida ili nanyi muweze kulipa kodi stahiki serikalini”. Amesema Dk. Kalemani.
Pamoja na kufunga transfoma moja kubwa yenye uwezo wa KVA 315, Waziri huyo ameiagiza Tanesco kufunga transfoma nyingine tatu hadi itakapofika mwisho wa Mei mwaka huu na moja iliyosalia ifungwe Juni. Pia ametoa wito kwa wachimbaji hao kuchangamkia umeme wa REA unaounganishwa kwa gharama ya Sh. 27,000
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa wachimbaji wa Nyakafuru, Walwa Katemi ameishukuru serikali kwa kuleta umeme eneo hilo.