Home BIASHARA Bora kuanzisha biashara au kuinunua?

Bora kuanzisha biashara au kuinunua?

0 comment 115 views

Siku zote mtu akipata wazo la biashara huwa na malengo makubwa ya kuendeleza wazo hilo kwa vitendo, na mwisho wa siku kunufaika na biashara hiyo. Kila siku biashara zinafunguliwa lakini sio zote hufanikiwa. Ni muhimu kutafari kutokana na mtaji ulionao; Je, kuna umuhimu wa kuanzisha kitu kipya au kuwekeza na kuendeleza biashara ambayo ipo tayari?

Kuanzisha biashara siku zote huhitaji mchakato sahihi ili kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa. Mfano ukiwa unataka kuanzisha biashara unatakiwa kufikiria eneo la biashara, sehemu ya kupata bidhaa, vibali, wafanyakazi na mambo mengine mengi. Hivyo sio jambo rahisi. Unatakiwa kuangalia uwezo ulionao kuhusu mchakato mzima wa kuanzisha biashara ili kujua kama utaweza au ni bora ukawekeze katika biashara ambayo imeshaanzishwa tayari. Ifahamike kuwa sio kila mjasiriamali au mfanyabiashara ana uwezo wa kuanzisha biashara na kuikuza.

Kwa upande mwingine, kuwekeza katika biashara ambayo imeshaanzishwa inakupa fursa ya kujihusisha na jambo ambalo lipo, biashara ambayo ishapata wateja, mapato, uhusiano wa biashara husika na wateja n.k. Kwa ujumla unakuwa na upeo wa nini kifanyike ili kuendeleza biashara hiyo na kunufaika pia kwa sababu mfanyabiashara wa awali anakuwa ameshaweka msingi wa biashara hiyo, na kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake, anashindwa kuendeleza biashara yake na hapo ndipo huhitaji kuuza biashara hiyo kwa mtu mwingine.

Faida ya biashara iliyoanzishwa ni kwamba kila kitu kinakuwa tayari kimewekwa na mfanyabiashara wa awali. Mfanyabiashara mpya hutakiwa tu kutimiza makubaliano stahiki. Kwa mfano mfanyabiashara wa awali anaweza kutaka kiasi fulani ili kuweza kuuza biashara pamoja na nyaraka, wafanyakazi hivyo mfanyabiashara mpya hatopata shida ya kuanza kutafuta wafanyabiashara na wateja. Yeye atajihusisha na kuinua kampuni na kuhakikisha anapata faida.

Pia ni muhimu kufanya maamuzi sahihi ikiwa unataka kununua au kuanzisha biashara. Kuna biashara ukianzisha unaweza kutopata faida kwa muda mrefu hivyo kukata tamaa. Vilevile, kununua biashara kwa mtu maana yake unanunua mambo mazuri na mabaya. Ikitokea umenunua biashara kwa mtu ambaye ana sifa ya lugha mbaya kwa wateja, unatakiwa uwe na uhakika kwamba utaweza kubadilisha mawazo ya wateja. Ikiwa unajua kwamba itakuchukua muda mrefu kurudisha uaminifu kwa wateja basi fanya maamuzi mengine.

Aidha, ni rahisi kupata mtaji kwenye biashara ambayo ipo tayari kuliko biashara ambayo ndio kwanza inaanza kwa sababu ukiwa unamuelekeza mtu akupe fedha kwa kitu anachokiona ni rahisi kwa mtu huyo kufanya tathmini ya faida inayoweza kupatikana, lakini kama hana uhakika mawazo yako yanaweza kuleta faida hapo mbeleni inakuwa ngumu kukupa mtaji ndiyo maana ukiwa unataka kuanzisha biashara yako, ni muhimu kuwa na mtaji ili kuepuka changamoto kama hizo.

Ukweli ni kwamba, kununua biashara kwa mtu ni gharama kubwa. Ikiwa una mpango huo hakikisha una fedha ya kutosha ya kufanya hivyo kwa sababu mfanyabiashara wa awali hawezi kuuza operesheni nzima ya biashara yake kwa bei rahisi.

Unashauriwa kuongea na wataalamu wa mambo ya biashara na uwekezaji kabla ya kufanya maamuzi sahihi kwani watakushauri kutokana na uzoefu wao na hali halisi ya biashara kwa kipindi hicho.

 

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter