Na Mwandishi wetu
Mauzo ya hisa katika Soko la Hisa la Dar es salaam yamepungua licha ya idadi ya hisa zilizouzwa kuongezeka kutoka hisa 600,000 hadi hisa 1.4 milioni kwa wiki iliyoishia Agosti 11. Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) imeongoza kwa mauzo ya asilimia 90.
Wiki chache zilizopita benki za biashara hapa nchini zilitoa taarifa za hesabu za fedha huku faida ikionekana kupungua. Baada ya kodi ya benki, faida ya CRDB imepungua mpaka 13.3 bilioni huku faida ya NMB ikishuka hadi 35.293 bilioni, yote haya katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka.
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Udalali ya Orbit Securities, Simon Juventus amesema kuwa suala la kupungua kwa faida sio la benki hizi tu bali imetokea kwa sekta nzima ya benki na fedha. Ameongeza kuwa CRDB imeanza mwaka vibaya lakini bado watu wana imani nayo inaweza kumaliza vizuri mwisho wa mwaka.
Aidha, ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa DSE umepungua kutoka Sh 18.3 trilioni hadi Sh 17.7 trilioni kwa wiki iliyoisha Agosti 4 kutokana na kushuka kwa bei ya hisa ya Shirika la Ndege la Kenya kwa asilimia 22, Uchumi Supermarket Limited kwa asilimia 14, Kampuni ya Bia ya Afrika Mashariki kwa asilimia 8 na Benki ya CRDB kwa asilimia 5.