Unaweza kufikiria kwamba kuanzisha biashara mtandaoni ni jambo rahisi. Ukweli ni kwamba, biashara nyingi za mtindo huu hushindwa kutengeneza faida ya aina yoyote na badala ya muda wamiliki wanalazimika kuzifunga.
Kuna sababu mbalimbali zinazoweza kufanya biashara za mtandaoni kushindwa kuendelea na moja kati ya sababu hizo ni kushindwa kufanya utafiti wa bidhaa zenye faida sokoni. Wafanyabiashara wanatakiwa kufanya utafiti wa kina ili kugundua soko linakosa bidhaa gani zenye uhitaji mkubwa kwani kwa kufanya hivyo, wanapata mwanga wa nini hasa wateja wanahitaji ili kuhakikisha kuwa wanaweka sokoni bidhaa sahihi
Biashara za mitandaoni zinatakiwa kuzingatia misingi ifuatayo ili kutengeneza faida na kujiweka katika nafasi nzuri ya kuendelea kutoa huduma kwa muda mrefu.
- Tatua tatizo la msingi
Kama ilivyo kwenye wazo la biashara, biashara ya mtandaoni inatakiwa kulenga kutatua tatizo lililopo. Unaweza kupata wazo bora zaidi kwa kuangalia mazingira yako, kuzungumza na majirani, ndugu pamoja na marafiki, kufanya utafiti kwenye mitandao mbalimbali kuona wafanyabiashara wengine wanakumbwa na changamoto gani ili biashara yako ije na suluhisho na kuwa katika nafasi nzuri zaidi sokoni.
- Chunguza washindani wako
Ukweli ni kwamba, unapofikiria kuanzisha biashara kuna uwezekano kwamba tayari kuna watu wanafanya biashara hiyo. Hii haimaanishi kwamba unatakiwa kuachana na wazo hilo bali uncahotakiwa kufanya ni kuendesha utafiti wa kina ili kujua ni kitu gani unaweza kufanya tofauti na kuwavutia wateja. Kwa kufanya hivi unaingia kwenye biashara ukiwa na muelekeo maalum ambao utakutambulisha vizuri kwenye soko.
- Angalia kitu gani kinavutia sokoni
Mara nyingi ni vigumu kutengeneza faida yoyote kama utachukua wazo ambalo ambalo tayari lipo na kuanzisha biashara. Lakini unachambua wazo hilo huku ukiwa umezingatia bidhaa au vitu ambavyo vinawavutia wateja, unaweza kuanzisha biashara yenye mafanikio makubwa. Tumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii kuangalia ni vitu gani wateja wanapendelea kwa wakati huo ili uwekeza kwenye bidhaa na huduma sahihi ambazo una uhakika zitafanya vizuri.
- Bei
Ni kitu kimoja kuuza bidhaa mtandaoni lakini ni kitu kingine kabisa kuuza bidhaa hiyo kwa faida. Wakati unapangilia bei, ni vizuri kuzingatia aina gani ya wateja ulionao. Jiulize, bidhaa hii itauza kwa bei hii? Wateja wangu wanaweza kumudu? Ni muhimu kupanga bei kwa kuzingatia uwezo wa wateja wako. Kwa mfano kama wateja wako wakubwa ni wanafunzi wa vyuo, basi bei zinatakiwa kuwa rafiki kwani kundi hili huzingatia sana bajeti kwa kuwa bado hawana uwezo wa kujitegemea.
- Fanya kitu unachopenda
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizofanywa duniani, wamiliki wengi wa biashara za mitandaoni wameeleza kuwa sababu ya kuanzisha biashara zao ni mapenzi waliyonayo kwa kitu hicho. Tofauti na wale walioanzisha biashara ili kutengeneza fedha, uhuru wa kufanya kazi sehemu yoyote n.k, wafanyabiashara wanaopendelea kile wanachofanya hufika mbali zaidi kwani msingi wako mkubwa ni upendo walionao kwa huduma au bidhaa wanayotoa.
Ni muhimu kupenda kitu ambacho unafanya kwani bila ya hivyo, utakosa hamasa ya kujituma zaidi ili kuhakikisha kuwa biashara yako inazaa matunda.
Mitandao ni sehemu nzuri kwa biashara kwa kuwa soko ni pana zaidi na unaweza kuwafikia watu wengi ndani ya muda mfupi tu. Mitandao ya kijamii kama Facebook na Instagram inaendelea kurahisisha mahusiano ya wateja na wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali ndani na hata nje ya nchi. Kama unafikiria kuanzisha biashara hakikisha unazingatia misingi hii ili kufikia malengo yako. Ni kweli kuwa biashara nyingi zimeshindwa kujiendeleza lakini ukisimama katika misingi imara, mitandao ina mchango mkubwa katika maendeleo.