Kila mtu huwa na ndoto za kuwa mtu fulani katika jamii, lakini sio wote hutimiza ndoto hizo kutokana na sababu mbalimbali. Familia na watu wa karibu wanaweza kumhamasisha mtu kutimiza ndoto zake ingawa sio kweli kuwa kila aliyefanikiwa hupata ushirikiano kutoka kwao.
Rajab Abdul Kahali maarufu kama Harmonize au “Kondeboy” ni mmoja wa watu maarufu ambao watu wanatakiwa kujifunza kutoka kwao. Harmonize hakukata tamaa na alipigania ndoto yake ya usanii japokuwa baba yake hakufurahishwa na njia ambayo alikuwa anataka kujipatia fedha.
Inaelezwa kuwa Harmonize mwenye miaka 25 amezaliwa mkoani Mtwara katika kijiji cha Chitoholi. Baada ya kumaliza sekondari aliamua kwenda Dar es salaam kutafuta maisha ambapo kwa kuanza alikuwa akijishughulisha na ubebaji wa maji na kuuza kahawa maeneo ya Kariakoo ili kujikimu kimaisha.
Safari yake ya muziki ilianza rasmi mwaka 2011 ambapo alitoa nyimbo kadhaa lakini hazikupata mashabiki wengi. Mwaka 2015 alikutana na Diamond Platnumz, msanii maarufu nchini. Wawili hao wakaanza kufanya mziki pamoja chini ya lebo ya WCB (Wasafi Classic Baby) na hapo ndipo ndoto za Harmonize zikaanza kutimia.
Haikuwa kazi rahisi kwa Harmonize kufikia alipo sasa kwani kipindi anapoanza kuimba chini ya WCB mashabiki wengi walikuwa hawafurahishwi na uimbaji wake, wengi walikuwa wakisema kuwa anaiga sauti ya Diamond Platnumz. Licha ya madai hayo kutoka kwa mashabiki, Harmonize hakurudi nyuma na akaendelea kusonga mbele na kutengeneza nyimbo zaidi ili kuwaonyesha mashabiki kuwa alizaliwa kufanya muziki na sio kitu kingine.
Baadhi ya nyimbo zilizomletea umaarufu zaidi na mafanikio makubwa mwanamuziki huyo ni pamoja na Aiyola, Happy Birthday, Bado, Kwangwaru, Atarudi, Paranawe na Never give up. Kibao chake kinachotamba zaidi hivi sasa ni Magufuli.
Kupitia muziki, Harmonize amejipatia mafanikio mengi ikiwa ni pamoja na kumiliki lebo ya muziki iitwayo Kondegang ambayo licha ya muziki imekuwa ikiwapa fursa vijana wenye mawazo mbalimbali na kuwasaidia kuyafanyia kazi ili waweze kutoka mtaani. Pia hivi karibuni, Harmonize ameonyesha msisitizo wake wa kuendeleza tasnia ya muziki ikiwa ni pamoja kuwasaidia wasanii wakongwe ambao wamepotea katika tasnia hiyo kutokana na sababu mbalimbali ambapo aliamua kumsaidia mwanamuziki wa muda mrefu Abubakar Katwila maarufu kama “Q Chief” kuendelea na muziki huku akiwa ameshafanya kolabo kadhaa na msanii Dully Sykes.
Kupitia kwa Harmonize, ni muhimu kwa kila mtu kujua ni ndoto gani anataka kutimiza katika maisha yake, kutambua uhalisia wa kuzitimiza ndoto hizo ili kuepukana na upotevu wa muda katika masuala yasiyowezekana, kutafakari na kutathmini mahali pa kuanzia ili kurahisisha utengenezaji wa mpango madhubuti utakaosaidia kutimiza ndoto hizo.
Haitakuwa rahisi na lazima utapitia vikwazo vingi lakini kujua nini hasa unataka ndio kutafanya ufanikiwe katika maisha.