Miundombinu bora ni muhimu kwa nchi yoyote inayotaka kupata maendeleo ya kiuchumi. Hata nchi zilizoendelea zimekuwa zikifanya kila jitihada na kuhakikisha wanakuwa na miundombinu bora ili shughuli zote za kiuchumi zifanyike kwa urahisi ba haraka zaidi. Ili kupata mafanikio ni muhimu kuhakikisha kila kitu kinafanywa vizuri kwa muda mchache.
Mataifa mbalimbali Afrika yamekuwa yakiungana ili kuweza kusaidiana katika mambo mbalimbali ikiwemo masuala ya biashara na maendeleo. Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) hufanya biashara kwa urahisi zaidi kutokana na masharti rafiki yaliyopo, lengo likiwa ni kuimarisha mahusiano ,kukuza uchumi na kuchochea maendeleo.
Mikutano ya jumuiya inalenga kutathmini mambo ambayo yamefanyika na mambo ambayo hayajafanyika baina ya wanachama, kisha kuorodhesha changamoto,vikwazo vilivyopelekea mambo hayo kutokufanyika na nini kifanyike ili kuondoa vikwazo na changamoto hizo ili kuendeleza uhusiano mzuri baina ya wanachama na wakati huo huo kuleta maendeleo.
Mwaka huu, mkutano wa SADC ulipangwa kufanyika nchini, na hivi sasa unaendelea kufanyika. Baadhi ya mambo ambayo yamegusiwa katika mkutano huo ni pamoja na masuala ya viwanda, uwekezaji, vijana huku vikao vikiwa vinaendelea kufanyika.
Kuhusu suala la biashara Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwanda na Biashara katika Sekretarieti ya SADC, Calicious Tutalife ameeleza wakati wa kikao hicho kuwa ikilinganishwa na kanda nyingine duniani, biashara iko chini katika kanda ya SADC na Afrika. Moja ya sababu iliyotajwa kuchochea hali hiyo ni miundombinu mibovu. Jumuiya hiyo imepanga kuanzisha mfuko wa pamoja wa maendeleo ya miundombinu ili kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya viwanda.
KITAKACHOTOKEA..
Kutokana na maboresho ya miundombinu yatakayofanyika, ni dhahiri kuwa uchumi baina ya wanachama wa SADC utakua kwa kasi na maendeleo yatakuwa ya pamoja. Watu wengi watafanikiwa kwa muda mmoja, jambo litakalosababisha umasikini upungue na watu wa kipato cha chini kupungua. Kwa mfano kama watu waliokuwa wakinufaika walikuwa ni wafanyabiashara wakubwa peke yake, kupitia maboresho ya miundombinu hata wazalishaji watanufaika zaidi kwani watakuwa na uwezo wa kusafirisha bidhaa zao wenyewe kutoka sehemu wanapozalisha hadi sokoni.
Watu wengi hasa wanaoishi vijijini hukata tamaa ya kuzalisha bidhaa nyingi kutokana na miundombinu mibovu. Kupitia marekebisho yatakayofanyika, watu hao wataweza kuzalisha zaidi kwa sababu watakuwa na uhakika wa kuyafikia masoko na kupata faida.
Miundombinu mibovu husababisha watu watumie gharama za ziada, muda na nguvu nyingi ili kuweza kukamilisha michakato yao ya biashara. Kutokana na maboresho yatakayofanyika, hali hayo itarahisishwa na kuruhusu watu kuelekeza juhudi katika kuzalisha na kulifikia soko kwa haraka zaidi.
Miundombinu bora siku zote huhamasisha wawekezaji kuwekeza hivyo maboresho yatakayofanyika yataruhusu wanachama kujiandaa na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwani maboresho ya miundombinu yatawafanya wengi zaidi wachangamkie fursa zilizopo.
Hivyo kupitia mkutano huu wanachama wa SADC hasa Tanzania wanatakiwa kujifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuchangamkia fursa mbalimbali zinazokuja na mkutano huu, ili kuleta maendeleo kupitia biashara za ndani na nje kuelekea uchumi wa viwanda.