Wakati mkutano wa SADC unaendelea nchini, imebainishwa kuwa ukanda huu una kiwango cha chini katika masuala ya biashara ikilinganishwa na kanda nyingine Afrika. Kwa upande wa Tanzania, mambo sio mabaya na kwa mujibu wa ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya mwaka 2017/18 uchumi wa nchi umekua kwa asilimia 7.1, licha ya michakato ya kibiashara baina ya wanachama wa SADC kupungua na kufikia asilimia 3.5 mwaka 2017.
Baadhi ya mambo ambayo yamejadiliwa ili kuongeza kasi ya masuala ya biashara ni pamoja na ubora na viwango vya bidhaa zinazozalishwa nchini kwa ajili ya kuuzwa katika masoko ya nje.
Pia wameongelea masuala ya vizuizi visivyo na ushuru, ambavyo vinaendelea kuwa changamoto katika biashara baina ya wanachama wa SADC. Kuna umuhimu wa serikali yetu kupitia upya baadhi ya vizuizi hivyo ili kurahisisha ushirikiano na kuchochea maendeleo ya kiuchumi. Kuhusu vibali vya usafirishaji, kumekuwa na mlolongo mrefu na ucheleweshaji wa mchakato mzima wa biashara jambo ambalo limekuwa likikwamisha biashara.
Hata hivyo, usafirishaji na uwepo maeneo ya kuhifadhi bidhaa ni baadhi ya mambo yanayosababisha uchumi wa Tanzania kukua. miundombinu ya bandari, reli na barabara ni baadhi ya mambo yanayosaidia uchumi.
Mbali na hayo, ili kupata matokeo chanya zaidi katika mkutano huu wa 39 wa Jumuiya ya SADC ushirikiano, umoja na maelewano ni baadhi ya mambo ambayo wanachama wanatakiwa kukubaliana nayo ili kuimarisha uchumi.