Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba amezitaka Taasisi za Huduma Ndogo za Fedha Daraja la pili kujiunga na taasisi mojawapo kati ya Mwamvuli wa Taasisi Zinazotoa Huduma Ndogo za Fedha (TAMFI) na Umoja wa Taasisi Zinazotoa Huduma Ndogo za Fedha( TAMIU) ifikapo mwishoni wa mwezi Desemba 2025.
Gavana Tutuba amesema hayo alipozindua Utaratibu wa Utekelezaji wa Hati ya Makubaliano ya Usimamizi Binafsi wa Sekta ya Huduma Ndogo za Fedha, kati ya Benki Kuu, TAMFI na TAMIU Julai 01, 2025 katika ofisi za BoT jijini Dar es Salaam.
“Taasisi zote za Huduma Ndogo za Fedha Daraja la pili zinalazimika kujiunga na chama kimojawapo kati ya TAMFI au TAMIU ndani ya kipindi cha miezi 6 na zoezi hili linatakiwa kuanza kutekelezwa kuanzia leo tarehe 1 Julai hadi mwishoni mwa Desemba 2025. Taasisi ambayo itakuwa haijajisajili kufikia Desemba tutainyang’anya leseni”. Amesema Gavana Tutuba.
Aidha, Gavana amesema kuwa utaratibu huu wa usimamizi binafsi utahakikisha TAMFI na TAMIU zinasimamia utendaji wa taasisi zinazotoa huduma ndogo za fedha kwa kuzingatia kanuni zilizopo kwa lengo la kutokomeza changamoto mbalimbali katika sekta hiyo ikiwemo Mikopo Umiza.
“TAMFI na TAMIU watakuwa na wajibu wa kusimamia mwenendo wa wanachama wao kwa kuzingatia kanuni bora za kimaadili, kuhamasisha utoaji wa elimu ya fedha kwa wateja, kusimamia na kuratibu mifumo ya kushughulikia malalamiko, Kuweka taratibu za uwajibikaji na uwazi katika utoaji wa huduma, na Kuwezesha utekelezaji wa kanuni na miongozo ya kiserikali,” Amesema.
Ameongeza kuwa Benki Kuu itaendelea kusimamia sekta hiyo kupitia utekelezaji wa sera, utoaji wa leseni, ulinzi kwa watumiaji wa huduma za fedha, ufuatiliaji wa mwenendo wa jumla wa sekta, na itahakikisha inashirikianiana kwa karibu na vyama hivyo ili kuhakikisha kwamba misingi ya makubaliano hayo yanatekelezwa kikamilifu.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya TAMFI, Devotha Minzi pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha TAMIU, Bw. Juma Mnanka, wameipongeza Benki Kuu kwa kuja na utaratibu huu na wameahidi wataendeleza ushirikiano ili kuhakikisha sekta hiyo inaimarika.