Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Marianne Young, katika ofisi za Benki Kuu jijini Dar es Salaam, tarehe 29 Aprili 2025.
Katika mazungumzo hayo, Gavana Tutuba alieleza kuwa uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika licha ya changamoto mbalimbali za kiuchumi duniani. Alibainisha kuwa kwa kipindi kinachoishia Desemba 2024, uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.5, hali inayoonesha ustahimilivu wa kiuchumi wa taifa.
Aidha, Gavana Tutuba alifafanua kuwa kuimarika kwa uchumi kumeambatana na kudhibitiwa kwa mfumuko wa bei, ambao ulifikia asilimia 3.1 kufikia Desemba 2024.
Aliongeza kuwa sekta ya fedha nchini inaendelea kukua kwa kasi, huku Benki Kuu ikiimarisha juhudi za kuongeza huduma jumuishi za fedha kwa wananchi wote, ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanatumia mifumo rasmi ya fedha na kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Balozi Young alipongeza juhudi za Benki Kuu katika kusimamia uchumi wa nchi. Alisisitiza kuwa Uingereza itaendelea kushirikiana na BoT katika masuala ya uchumi na fedha, sambamba na kukuza maendeleo endelevu ya Tanzania.

Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Marianne Young
Miongoni mwa waliohudhuria kikao hicho ni Naibu Gavana wa Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayandabila, Naibu Gavana wa Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo, pamoja na maafisa waandamizi kutoka menejimenti ya Benki Kuu ya Tanzania.