Home BENKI Naibu Waziri Mkuu Dkt. Biteko azitaka benki kutembelea wakulima

Naibu Waziri Mkuu Dkt. Biteko azitaka benki kutembelea wakulima

0 comment 45 views

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewataka wenye benki nchini kuwekeza zaidi kwa kuwafuta wakulima na wafugaji na kuwavutia kupata huduma za kibenki.

Dkt. Biteko amesema hayo Agosti 12, 2024 wakati hafla ya uzinduzi wa tawi la Benki ya KCB wilayani Geita.

“Watembeleeni wakulima, wakulima ni kundi kubwa ambalo benki nyingi zinawakimbia, lakini ndio eneo ambalo ajira kwa Watanzania ni zaidi ya asilimia 70, kwa maneno mengine kama kuna biashara kubwa ya kufanya, sio tuu kwenye madini, lakini kwenye kilimo ambapo watu wengi hawajapata msukumo mkubwa kama benki kwenda kuwasaidia wakulima,” amesisitiza Dkt. Biteko.

Amesema kuwa licha ya benki ya KCB kuvutia huduma zao kwa wafanyabiashara wavutie pia wakulima na wafugaji kwa kuwa ndilo kundi kubwa ambalo bado linakabiliwa na changamoto za huduma za mikopo katika benki mbalimbali nchini.

“ Nimefarijika kuona KCB imefungua tawi Geita na kusogeza huduma za kibenki kwa wananchi hii itasaidia kuchochea uchumi kwao na mjue mko mahali ambapo wananchi wake wanafanyakazi kwa bidii, wanalima, kufuga kwa bidii na wafanyabiashara wanafanya biashara kwa bidii na wengine wako sekta ya madini,” amesema Dkt. Biteko.

“ KCB imetoa zaidi ya shilingi bilioni 329.7 kwa Wakala wa Nishati Vijini (REA) ambazo wamekopa wakandarasi ili kupeleka umeme vijijini ambapo umefikia asilimia 95, shilingi bilioni 107.1 kwa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) pamoja na kutoa shilingi bilioni 103.9 kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa ajili ya ujenzi wa barabara katika maeneo mbalimbali, amesema Dkt. Biteko

Vilevile, Mkurugenzi wa Kanda wa Biashara na Mkuu wa KCB Benki Tanzania, Cosmas Kimario amesema kuwa benki hiyo imeendelea kukua na kuendeleza uwekezaji wake wa biashara za kibenki katika maeneo mbalimbali nchini na kuwa sasa ina zaidi ya miaka 25 na matawi 17.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter