Home BENKI NMB yarudisha milioni 60 kwa jamii

NMB yarudisha milioni 60 kwa jamii

0 comment 42 views

Benki ya NMB imetoa msaada wa takribani Sh. 60 milioni unaohusisha vifaa vya afya, mabati, madawati na mbao katika wilaya za Korogwe na Kilindi mkoani Tanga. Kaimu Meneja wa benki hiyo kanda ya kaskazini Cosmas Sadat amesema NMB imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia miradi mbalimbali yenye kuleta maendeleo kwa wananchi hususani ile ambayo imekijita kwenye sekta za elimu na afya.

“Tunatambua kuwa ni kupitia jamii ndipo wateja wetu wengi wanapotoka, hivyo kurudisha sehemu ya faida kwa jamii ni utamaduni wetu, kwa maana hiyo tumeamua kushirikiana na serikali ya wilaya za Korogwe na Kilindi na kuwapatia madawati zaidi ya 200, vifaa vya tiba na vifaa vya ujenzi kwa shule zaidi ya 10 na hospitali kuonyesha kuwa tunajali”. Ameeleza Sadat.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Sauda Mtondoo amesema msaada huo waliopatiwa na NMB utasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha miundombinu ya shule pamoja na afya za wananchi. Naye Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Kasongwa ameishukuru benki hiyo kwa msaada waliotoa na kusema umewasaidia katika kupambana na changamoto za uhaba wa madawati na vifaa vya ujenzi.

Baadhi ya shule zitakazofaidika na msaada huo ni pamoja na Shule ya Msingi Mtonga, Shule ya Sekondari Semkiwa, Sekondari ya Wasichana Korogwe pamoja na Shule ya Msingi Kwamngumi. Katika upande wa sekta ya afya, zahanati mbili zimepatiwa vifaa tiba vyenye thamani ya Sh. 30 milioni.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter