Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeamua kuendelea na kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) cha asilimia 6 kwa robo ya pili ya mwaka 2025.
Akizungumza mbele ya wakuu wa benki na taasisi za fedha pamoja na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Yamungu Kayandabila, alitangaza uamuzi huo kufuatia kikao cha Kamati kilichofanyika Aprili 03, 2025.

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Yamungu Kayandabila.
“Uamuzi huu wa Kamati unalenga kuukinga uchumi dhidi ya athari zinazoweza kutokea kutokana na vikwazo vya kibiashara na migogoro ya kisiasa duniani,” alisema Dkt. Kayandabila.
Aidha, ameeleza kuwa Benki Kuu itaendelea kutekeleza sera ya fedha ili kuhakikisha mfumuko wa bei na kasi ya ukuaji wa uchumi nchini vinabaki ndani ya malengo na riba baina ya benki inabaki ndani ya wigo wa asilimia 4-8.
Kuhusu mwenendo wa uchumi nchini, Kamati ya Sera ya Fedha imesema ripoti za utafiti kuhusu mtazamo wa soko (Market Survey Perception), maoni ya wakuu wa kampuni mbalimbali nchini pamoja na tathmini iliyofanywa na kampuni ya Moodys mwezi Machi 2025, Tanzania ilibakizwa katika Daraja B1 ikiwa na mwelekeo imara.
Aidha, mazingira ya uchumi duniani katika robo ya kwanza ya mwaka 2025 yaliimarika, ambapo shughuli za kiuchumi katika nchi zilizoendelea na zile zinazoibukia kiuchumi ziliendelea kuimarika. Mwenendo huu unatarajiwa kuendelea katika robo zijazo za mwaka 2025.
Hata hivyo, matarajio hayo mazuri ya uchumi yanaweza kuathiriwa endapo vikwazo vya kibiashara na migogoro ya kisiasa duniani itaongezeka, ameeleza Dkt. Kayandabila akisoma ripoti hiyo ya Kamati ya Sera ya Fedha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabenki nchini (TBA), Theobald Sabi ameipongeza Benki Kuu na Serikali kwa ujumla kwa kuendelea kusimamia vizuri uchumi wa nchi na ameishukuru BoT kwa ushirikiano mzuri kwa mabenki nchini ambao una mchango katika ustawi wa sekta ya fedha nchini.