Home BENKI Riba ya Benki Kuu ya Tanzania yapungua kutoka asilimia 6 hadi 5.75

Riba ya Benki Kuu ya Tanzania yapungua kutoka asilimia 6 hadi 5.75

0 comments 38 views

Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeshusha kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) kutoka asilimia 6 hadi asilimia 5.75 katika robo ya tatu ya mwaka inayoanza Julai hadi Septemba 2025.

Kiwango cha Riba cha Benki Kuu (CBR) ni kiwango kinachotumika na BoT katika shughuli zake na benki za biashara, ambazo zinapaswa kufuata sera hiyo ndani ya wigo wa asilimia ±2.0 ya kiwango kilichowekwa.

Akizungumza katika mkutano wa viongozi wa benki na waandishi wa habari, Gavana wa BoT ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha, Emmanuel Tutuba amesema uamuzi huu unatokana na mwenendo mzuri wa kuimarika kwa shughuli za kiuchumi na udhibiti wa mfumuko wa bei.

‘Uamuzi huu unaakisi imani ya Kamati katika mwenendo wa mfumuko wa bei ambao umeendelea kubaki ndani ya wigo wa asilimia 3–5. Hali hii inatokana na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti, kuanza kwa msimu wa mavuno, pamoja na utulivu wa thamani ya shilingi ya Tanzania,” amesema Gavana Tutuba.

Ameongeza kuwa , Benki Kuu itatekeleza sera ya fedha ili kuhakikisha riba ya mikopo ya siku saba baina ya benki (7-day interbank rate) inabaki ndani ya wigo wa asilimia 3.75 hadi 7.75.

Kuhusu mwenendo wa uchumi wa nchi, Gavana amesema umeendelea kuimarika ukichochewa na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika miundombinu na kuongezeka kwa shughuli za sekta binafsi, kutokana na kuimarika kwa mazingira ya ufanyaji biashara.

Aidha, amesisitiza kuwa hatari za misukosuko ya nje kwenye matarajio ya mwenendo wa uchumi ni ndogo, kutokana na muundo wa uchumi wa nchi ambao unategemea sekta mbalimbali za uzalishaji, pamoja na utekelezaji thabiti wa sera na programu zinazochochea ukuaji wa uchumi, ambazo zinatarajiwa kusaidia kuhimili misukosuko hiyo.

Akijibu swali la mwandishi wa habari, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabenki Tanzania, Theobald Sabi, alisema kuwa kupungua kwa CBR kunaweza kuchangia kupunguza viwango vya riba vinavyotozwa na benki za biashara. Hata hivyo, viwango hivyo huathiriwa pia na vigezo vingine kama vile nguvu za soko na tathmini ya vihatarishi inayofanywa kwa mteja kabla ya kumpa mkopo.

Oktoba 2024, Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilisema Riba ya Benki Kuu (CBR) kwa kwa robo ya mwisho wa mwaka 2024 itabaki kuwa asilimia sita.

Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba alieleza hayo jijini Dodoma kuwa uamuzi huo umeafikiwa kutokana na matarajio ya mfumuko wa bei kuendelea kuwa chini ya lengo la nchi la asilimia 5.

Tangu robo ya pili ya mwaka 2024 kiwango hicho cha riba kimebakia kuwa asilimia sita baada ya kuongezwa kidogo mapema mwezi Aprili.

Alibainisha kuwa “kamati pia inatarajia uchumi kuendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha, sambamba na kuimarika kwa mazingira ya kiuchumi duniani.”

Kamati hiyo iliyoketi Oktoba 2, 2024 inatarajiwa kuwa uchumi wa dunia utaendelea kukua sambamba na kuimarika kwa mazingira ya upatikanaji fedha.

Gavana Tutuba alisema kuwa kamati ilibaini kuwa utekelezaji wa sera ya fedha ulifanikiwa kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki ndani ya lengo la asilimia 5.

Mfumuko wa bei Tanzania uliorekidiwa mwezi Julai kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) umeendelea kuwa imara ukiwa kati ya asilimia 3.0 na 3.2 ndani mwaka mmoja.

Aidha katika mwaka unaoishia Agosti 2024, mfumuko wa bei uliongozeka kidogo hadi asilimia 3.1 kutoka asilimia 3.0.

Alisema “katika robo ya kwanza ya mwaka 2024, uchumi ulikuwa kwa asilimia 5.6 huku shughuli za ujenzi, kilimo, fedha, bima na usafirishaji vikichangia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji huu.”

Kwa mujibu wa viashiria vy awali, alieleza kuwa uchumi unakadiriwa kukua kwa 5.8% na 5.6% katika robo ya pili nay a tatu ya mwaka 2024, mtawalia na unatarajiwa kuendelea kukua katika viwango hivyo katika robo ya mwisho wa mwaka.

Ukuaji huo unatarajiwa kuchangiwa zaidi na kuendelea kuimarika kwa mazingira ya kiuchumi nchini kutokana na maboresho katika uwekezaji na biashara na kuboreka kwa uchumi wa dunia.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!