Home BIASHARA Maganda ya korosho yanavyotengeneza mafuta

Maganda ya korosho yanavyotengeneza mafuta

0 comment 234 views

Kama ulikuwa hufahamu kuwa maganda yatokanayo na zao la korosho yanatengeneza mafuta, basi sasa ujue. Lydia Amor ni mjasiriamali katika Halmashauri ya Mji wa Masasi ambae pia ni Mkurugenzi wa Lige Enterprise alifika katika maonyesho ya 45 ya Biashara (sabasaba) na kuweza kuonyesha bidhaa mbalimbali ikiwemo zao la korosho.

“Nimefurahi sana kuweza kushiriki katika maonyesho haya mwaka huu, mbali na kuuza korosho pia tuna bidhaa nyingine itokanayo na zao hilo ambayo ni mafuta yajulikanayo kwa jina la CashewNut Shells Liquid (CNSL).

Mafuta haya yanatokana na maganda ya korosho, watu wengi walikuwa hawajui kama maganda ya korosho yanatengeneza mafuta.” ameeleza Lydia.

Akieleza jinsi ya kutengeneza mafuta hayo, amesema “korosho hii ambayo tunapata mafuta ni korosho inayochemshwa kitaalamu, ambapo kuna korosho zinazochemshwa kwa dakika saba hadi tisa kulingana na ukubwa wa korosho.”

Amesema baada ya zoezi la kuchemsha korosho huachwa zipoe kwa muda wa saa 24 ndipo hubanguliwa kutoa korosho na ganda.

“Kwanza tunapata faida kwenye korosho yenyewe na pili kwenye ganda. Tena naona kama maganda yana faida zaidi. Baada ya kutoa maganda huwa ninayapeleka kwenye kisima kwa ajili ya kutengeneza mafuta. Nilipata mafunzo kutoka Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) wakishirikiana na Bodi ya Korosho jinsi ya kupata haya mafuta ya maganda ya korosho” ameeleza.

“Nimejenga kisima mabacho kina tanuru kwa juu na kuweka mabomba kwa chini ambayo yatatumika kupitisha mafuta. Ninachofanya ni kuweka maganda katika kisima na kuyachoma ambapo jinsi yanavyowaka na kuteketea yanatoa mafuta.”

Amesema kwa hatua aliyofikia mafuta hayo yanaweza kutumika kuzuia mchwa na wadudu waharibifu wa mbao lakini mafuta hayo pia yanaweza kutengeneza vilainishi mbalimbali na rangi endapo yatapitishwa kwenye mitambo mikubwa.

“Watu wengi waliotembelea hapa wameshtuka na kuishangaa bidhaa hii, nimekuwa nikiwapa elimu na naona mwitikio ni mzuri na watu wameanza kununua na kwa kweli kuna uhitaji wa haya mafuta.”

Akizungumzia changamoto amesema mafuta hayo hayatengenezwi kwenye maeneo ya makazi kutokana na moshi hivyo humlazimu kusafiri umbali mrefu mbali na makazi ya watu.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter