“Ninaamini kuajiriwa ni utumwa, sipendi wala sitamani kuajiriwa,”. Haya ni maneno ya Andrew Mpambazi, kijana mwenye umri wa miaka 26 mweye stashahada ya sayansi ya computer kutoka chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mpambazi ambae anauza sabuni za kuogea anasema mara baada ya kumaliza elimu yake mwezi Julai 2019 hakufanikiwa kupata ajira.
“Nilisafiri mikoa takribani saba kuangalia fursa zilizopo nikiwaza nifanye biashara gani. Nilikuwa nina mtaji wa shilingi laki tatu, baada ya kuwaza sana nikapata wazo la kutengeneza sabuni za magadi,” anasema Mpambazi.
Kijana huyu ambae ni mzaliwa wa Mkoa wa Kigoma uliopo Kusi mwa Tanzania hakutamani kabisa kuajiriwa. Ndoto zake ni kujiajiri mwenyewe, tofauti na wahitimu wengi wanapomaliza masomo hutamani kupata ajira katika kampuni mbalimbali.
Baada ya kufanya utafiti juu ya biashara ya kutengeneza sabuni aligundua kuwa mtaji wake wa shilingi laki tatu ulikuwa hautoshi kuanzanisha biashara hiyo kwani inamlazimu mtu kuwa na wastani wa kiwango cha chini cha shilingi laki tano kufanya biashara hiyo.
“Nilizungumza na familia yangu wakanisaidia kuniongezea laki mbili, nikaanza kutengeneza sabuni za magadi Kigoma. Nilianza kutengeneza miche ya sabuni 280 na kuiuza maeneo mbalimbali mkoani Kigoma.
Nilitumia sana mtandao wa kijamii wa Twitter kufanya biashara yangu. Nilipata wateja wengi sana kupitia Twitter”.
Kwa mtaji wa laki tano, Mpambazi aliweza kuuza sabuni zake na kupata shilingi laki nane kwa kipindi cha wiki mbili.
Mpambazi anasema alipata mteja kutoka Sirali Mkoani Mara akimtaka ampelekee mzigo wa sabuni ambapo gharama za kutengeneza sabuni hizo ilikuwa shilingi milioni mbili.
“Sikuwa na milioni mbili, mama yangu alinikopea na kunipa hiyo fedha. Nikatengeneza sabuni na kwenda nazo Mara kumpelekea mteja. Nilifika mpaka hotelini na kuwasiliana na mtu aliehitaji mzigo wa sabuni. Bila kutegemea nilipowasiliana nae aliniambia kuwa biashara haiwezi kufanyika kutokana na mpaka kufungwa kwa sababu ya ugonjwa wa corona kwani sabuni alihitaji kuzisafirisha nchi jirani ya Kenya”.
Mpambazi anasema ilimlazimu kuanza kuuza sabuni zile rejareja ili walau apate fedha za kurudisha mtaji wake.
“Nilianza kuuza sabuni maduka ya jirani na stendi ya mabasi karibu na nyumba ya wageni nilipofikia, kuna duka nilikutana na kijana akaniambia nimkopeshe sabuni na baada ya siku mbili nifate malipo, nilipoenda akaniambia njoo tena baada ya siku tatu, nilipoenda tena sikumkuta kijana Yule. Niliambiwa ametoroka dukani na fedha zangu zaidi ya milioni moja.
Nilichanganyikiwa nisijue cha kufanya, nikaondoka Mara nikaenda Mwanza nikiwaza nini cha kufanya. Wakati huo kulikuwa na shindano la wazo la biashara lililokuwa linachezeshwa na Mo Dewji Foundation katika mtandao wa Twitter ambapo mshindi alikuwa anajinyakulia shilingi milioni moja. Nilishiriki na nikashinda milioni moja nikapata mtaji tena,” anasema Mpambazi.
Anaeleza kuwa hapo ndipo alipopata wazo la kutengeneza sabuni za matunda na kuzipa jina la “The Champ Mpambazi”.
“Nilitumia mtandao wa Twitter kutangaza sabuni zangu, watu walizipokea vizuri na sasa nina wateja wengi kupitia mitandao ya kijamii. Sina duka, ninatumia mitandao kuuza sabuni zangu tangu nilipoanza mpaka sasa na mikoani ninatuma.
Mpambazi anasema kupitia biashara yake sasa ameweza kuajiri watu takribani ishirini, ikiwa ni katika uzalishaji na wauzaji katika mikoa mbalimbali.
Akizungumzia changamoto anasema zipo katika utengenezaji sabuni kwani wanatengeneza kwa mikono.
Mpambazi anasema “fursa za biashara zipo nyingi sana, nawashauri vijana wasiwe wavivu badala yake waangalie fursa zilizopo na kuzifanyia kazi”.
Anasema ana ndoto za kufungua kiwanda mwakani ambapo atatengeneza bidhaa nyingine ikiwemo mafuta na sabuni nyingine.